“Viongozi wa dini wasiingilie siasa za upande mmoja”

Viongozi wa dini nchini wametakiwa kuepuka kuingilia siasa kwa namna yoyote, badala yake wajitahidi kuwa daraja la kuunganisha makundi mbalimbali yanayotofautiana kisiasa.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Islaah Islamic, Seif Sule ‘Dk. Sule’, ambaye amesema kuwa nafasi ya viongozi wa dini ni kutoa miongozo ya kimaadili na kiroho, siyo kushiriki katika migogoro ya kisiasa ambayo inaweza kuathiri amani na mshikamano wa taifa.

Amesema kuwa kiongozi wa dini si mpelelezi wa serikali, wala hana uwezo wa kufuatilia taarifa za kiusalama, hivyo haipaswi kutumia madhabahu na mimbari kutoa matamko ambayo yanaweza kugawanya umma.

Amesisitiza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuepuka upande mmoja wa kisiasa na badala yake wawe sehemu ya kujenga siasa za maridhiano na kuhamasisha mazungumzo na uvumilivu.

Akiwahimiza viongozi wa dini kutokuwa na msimamo wa kisiasa unaoegemea upande mmoja, Dk. Sule alikumbusha kuwa historia inaonyesha kuwa migogoro mingi inatokea pale ambapo viongozi wa dini wanajiingiza kwenye siasa za upande mmoja, akitolea mfano vurugu zilizotokea katika tukio la Mwembechai miama ya nyuma.

Amesema kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuwa mfano wa busara na utulivu katika kipindi cha uchaguzi, na kujiepusha na matamko ambayo yanaweza kuchochea machafuko.

Dk Sule amekumbusha kuwa siasa zinahitaji uhuru wa vyombo vya dola kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, bila kuingiliwa na matamko ya kisiasa.

Alisisitiza kuwa kama mtu hana hatia, mahakama itamwachia huru, lakini kama atapatikana na kosa, sheria itachukua mkondo wake.

Dk Sule ametoa wito kwa viongozi wa dini, vyama vya siasa na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanaheshimu amani ya nchi, kwa kuwa ni nguzo muhimu ya maendeleo na mshikamano wa kitaifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button