Vituo ukaguzi vyombo vya moto kujengwa mikoa 26

DAR ES SALAAM: MKATABA wa PPP wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 116 umesainiwa kati ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi na kampuni binafsi kwa ajili ya kujenga na kuendesha vituo vya ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, alisema mkataba huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 20 kupitia utaratibu wa ubia (PPP).
Amesema makubaliano hayo yamefikiwa kati ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Kampuni Maalum ya Utekelezaji wa Mradi ( Special Purpose Vehicle – SPV) inayojulikana kama MVI – TANZANIA.

Kampuni hii inaundwa na Ushirika wa Makampuni (Consortium) kutoka sekta binafsi ambao ni SAMA Exim DMCC na VIGOR.
Kwa mujibu wa Kafulila, mradi huo utahusisha matumizi ya teknolojia na vifaa vya ukaguzi vya kisasa kutoka kampuni ya DKT na MAHA kutoka Ujerumani huku uendeshaji wake ukisimamiwa na kampuni ya kimataifa ya APPLUS Automotive+ kutoka SPAIN.
Vilevile, Serikali kupitia Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi itakuwa na hisa asilimia 20 kwenye Kampuni Maalum ya Utekelezaji wa Mradi (MVI – TANZANIA).
Alisema huu ni mradi wa kwanza wa aina yake kwa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi kuingia ubia na sekta binafsi, jambo linaloashiria mabadiliko katika namna taasisi za umma zinavyotekeleza miradi ya maendeleo.
“Licha ya kuwa sekta ya usalama ingeweza kutekeleza mradi huu kwa kutumia fedha za serikali, uamuzi wa kuingia ubia unaonesha mwelekeo mpya wa kuvutia mitaji ya sekta binafsi,” alisema Kafulila.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza matumizi ya vyanzo mbadala vya fedha katika kugharamia miradi mikubwa.
Kafulila alisisitiza kuwa ubia huo si ubinafsishaji, bali ni ushirikiano wa pande mbili wenye lengo la kuboresha huduma, huku kituo cha ubia kikiiendelea kusimamia utekelezaji wake kwa mujibu wa sheria katika kipindi chote cha mkataba.



