Vituo vya SGR ‘dili’ kampuni ya simu ikifungua duka stesheni Dar

Miundombinu ya SGR yavutia kampuni kuwekeza

DAR ES SALAAM: Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2024, Vodacom Tanzania Plc leo imezindua duka jipya— Vodashop katika stesheni ya SGR iliyoko Jijini Dar es Salaam.

Hatua hii muhimu inaendana na kaulimbiu ya wiki ya huduma kwa wateja ‘Huduma Bora Kila Wakati’ ikionesha dhamira ya kampuni hiyo kutoa huduma stahiki kwa wateja wake huku wakipanua wigo wa upatikanaji kote nchini.

Ikiwa imepangwa kimkakati kuhudumia abiria wa treni ya SGR, duka hili jipya litakuwa kituo kinachotoa huduma zote za kampuni hiyo.

Advertisement

Wasafiri sasa wanaweza kupata huduma za kuongeza muda wa maongezi, huduma za M-Pesa pamoja na msaada wa wataalamu wa watoa huduma kwa wateja kwa urahisi, ili kuhakikisha wanaunganishwa na mtandao muda wote wa safari zao.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Plc, Philip Besiimire, alisisitiza umuhimu wa hatua hii, "tunafuraha kuzindua Vodashop hii iliyoko ndani ya stesheni ya SGR hapa jijini Dar es Salaam, hii ni hatua muhimu katika kuleta huduma zetu za viwango vya kimataifa karibu zaidi na wateja wetu.

Aidha, uzinduzi huu ni sehemu ya maono yetu mapana ya kuziba pengo la kidijitali kwa kutoa upatikanaji wa vifaa vya kisasa, mipango nafuu ya vifurushi, huduma za kifedha za simu pamoja na kuleta fursa za kidijitali karibu na kila mteja." Uzinduzi wa SGR Vodashop ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha huduma wakati wote wa safari kwa abiria wote wa treni inayopita katika reli ya viwango vya kimataifa (SGR).

Vodacom Tanzania tayari inapanua mtandao wake wa maduka na mipango ya kufungua maduka zaidi katika vituo vikuu vya Morogoro, Dodoma na Mwanza iko njiani.

SOMA: TCB yajivunia mafanikio mradi wa SGR

Maduka haya mapya yatatoa huduma ya viwango, yakirahisisha upatikanaji upatikanaji wa bidhaa na huduma mbalimbali za kampuni hiyo. Upanuzi huu unaendana na maono ya Vodacom ya kukuza ujumuishwaji wa kidijitali, kuimarisha muunganisho na kusaidia ukuaji wa kijamii na kiuchumi kote nchini.

“Kama sehemu ya uwepo wetu wa maduka nchi nzima, tunatambua kuwa wateja wetu pia wanategemea sana njia za kidijitali ili kuweza kujihudumia wenyewe popote walipo,” alisema Besiimire na kusisitiza: “Tumejidhatiti kutoa huduma ndani ya maduka na mtandaoni ili kuhakikisha kuwa wateja wetu hawapati changamoto yeyote wakati wa matumizi ya huduma zetu,” Mkurugenzi Mtendaji aliongeza.

Uzinduzi wa SGR Vodashop unathibitisha ahadi za Vodacom za kutoa huduma bora kwa wateja wakati wote pamoja na suluhisho za kibunifu na zenye kuzingatia mahitaji ya wateja ili kuboresha maisha ya Watanzania.

Wakati nchi inakumbatia mabadiliko ya kidijitali, Vodacom Tanzania inabaki kuwa taasisi yenye nguvu inayohakikisha kila mteja anaunganishwa katika mawasiliano kwa urahisi zaidi, na haswa hasa kwa wale walio safarini.