Vodacom wazindua huduma malipo kimataifa

DAR ES SALAAM; KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imezindua huduma ya malipo ya kimataifa, hatua inayoleta mapinduzi katika biashara na urahisi wa malipo kwa wateja na wafanyabiashara wa Tanzania wanaosafiri na kufanya biashara nje ya mipaka ya nchi.

Pia huduma hiyo inaongeza ujumuishwaji wa kifedha kidijiti.

Kupitia ushirikiano na VISA, Alipay, Network International, Magnati na MTN Uganda, wateja sasa wanaweza kufanya malipo kwa kutumia mfumo wa Tap & Pay duniani kote kwa kugusisha simu yenye M-Pesa Visa card kwenye mashine ya malipo.

Pia kulipa wafanyabiashara China kupitia Alipay kwa mfumo unaowezeshwa na Thunes, kufanya miamala Dubai kwa wafanyabiashara waliounganishwa kwenye mfumo wa TerraPay, pamoja na kuwalipa wafanyabiashara nchini Uganda moja kwa moja kwenye waleti zao za MTN MoMo. Yote haya kupitia M-Pesa Super App au Menyu ya M-Pesa.

Mkurugenzi wa M-Pesa Vodacom Tanzania, Epimack Mbeteni alisema, “Ushirikiano wetu na VISA, Alipay, Network International na MTN Uganda unaonesha dhamira yetu ya kujenga mifumo imara ya malipo ya kidijiti.

Kwa pamoja, tunawawezesha watu kufanya malipo hata wavukapo mipaka ya Tanzania kwa urahisi ule ule wanaoufanya ndani ya nchi, kwa usalama, haraka na kwa gharama nafuu,”.

Alisema huduma hizo ni salama, rahisi kutumia na zinaondoa changamoto zinazotokana na mifumo ya kibenki.

“Uzinduzi huu unawawezesha wateja wa Tanzania na wasafiri wanaofanya malipo ya mara kwa mara katika uwanda wa Afrika Mashariki, Mashariki ya Kati, Asia na maeneo mengine duniani, lakini hukabiliana na gharama, ucheleweshwaji au ukosefu wa usalama kwa baadhi ya mifumo ya malipo,” alisema.

Meneja wa Visa Tanzania, Victor Makere alisema: “Kupitia ushirikiano huu, tunawawezesha mamilioni ya wateja wa M-Pesa kufurahia malipo ya kidijiti yaliyo salama na rahisi popote Visa inapokubalika. Teknolojia ya Tap & Pay ni huduma inayomruhusu mteja kulipa kwa kugusisha simu yake karibu na mashine ya malipo yenye mfumo wa Visa, bila kuingiza namba ya kadi au PIN”.

“Kupitia ushirikiano wetu na Vodacom, sasa tunawezesha biashara za Tanzania kuwalipa wafanyabiashara wa China papo hapo kupitia mtandao wa Alipay. Kiwango hiki kipya cha uunganishaji na ubunifu kinaongeza imani katika mifumo ya kifedha ya simu na kufungua fursa mpya za biashara ya kimataifa”

Willie Kanyeki, Makamu wa Rais wa TerraPay Kusini mwa Jangwa la Sahara, alisema: “TerraPay tunaamini katika uunganishaji wa mifumo na kuwezesha malipo bila mipaka. Ushirikiano wetu na Vodacom unapanua fursa za biashara kwa njia salama, kwa Watanzania wanaofanya shughuli Dubai, na kuwaunganisha watumiaji wa Afrika na masoko mapya ya dunia.”

Mkurugenzi wa MTN Mobile Money Uganda, Richard Yego alisema: “Pamoja na Vodacom, tunafungua upatikanaji mkubwa wa huduma za kifedha kwa maelfu ya wafanyabiashara wanaovuka mipaka ya Uganda na Tanzania, hasa wale wa sekta ya biashara ndogo na za kati ambao ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu.”

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button