Vyama vyafundwa kupata wagombea
VYAMA vya siasa vimeshauriwa vizingatie mambo sita ukiwemo uwazi katika kupata wagombea ubunge na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Mambo mengine ni weledi, maadili, uzalendo, ushirikishwaji, matakwa ya wakati na kufahamu historia ya wanaoomba ridhaa ya kugombea nafasi hizo.
Mwanasiasa mkongwe na Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati alisema ni muhimu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiwe makini kwenye mchakato huo kutokana na wingi wa waliochukua fomu kuomba kugombea.
Chiligati alisema njia nyingine ya kupata mgombea bora ni kujichuja ili wale ambao uwezo wao umefika mwisho waondoke kupisha wenye uwezo waendelee kujenga nchi kupitia mawazo yenye ubunifu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha ADC na mgombea urais wa Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kupitia chama hicho, Hamad Rashid Mohammed alisema njia bora ya kupata mgombea safi wa ubunge ni kutafuta wazalendo na wenye uchungu na nchi yao.
“Njia nyingine ya kupata wagombea bora ni kujikita katika kupunguza pengo la wasio nacho na walionacho kwa kupata taarifa za umiliki wa mali za wagombea ili chama kisipeleke matajiri bungeni,” alisema Hamad.
Aidha, alisema vyama vya siasa lazima viwe makini katika kuwapitisha wagombea wao ili kuepuka kuwapitisha wanaotukana viongozi na wasioweza kujenga hoja kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Naye mwanasiasa mkongwe, Anna Abdalla aliwapongeza wabunge waliomaliza muda wao na kuamua kutochukua fomu za kuwania nafasi hiyo na akasema wamewajibika na wataheshimika kwa wananchi katika maisha yao yote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa na Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea, Juma Ali Hatibu alisema ni lazima vyama vya siasa vizingatie wagombea wenye maadili ya uongozi.
“Vyama vya siasa vinapopitisha wagombea wazingatie kwamba kwanza wawe wana uzalendo kwa nchi na wenye maadili ya uongozi,” alisema Hatibu.
Naye Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Loisulie alisema vyama vya siasa vinapaswa kuzingatia uwazi na ushirikishwaji wa umma katika mchakato ili ya kujenga imani kwa watia nia na kwa umma.
“Mchakato mzima watu wauelewe na wauthamini na kuufanya kama ni mchakato wao, kanuni ziwe wazi, mifumo iwe wazi na baada ya hapo mchakato lazima uwe shirikishi, lazima watu wajione ni sehemu ya huo mchakato,” alisema Dk Loisulie.
Alisema ikitokea kuna hujuma inayotokana na watu kutaka kutumia njia ya mkato na kuleta ‘ujanja ujanja’ weledi utumike katika kufanya uamuzi na kuwawajibisha wahusika kwa misingi ya haki.
“Baada ya mchakato wa ndani ya vyama unakuja ushindani na vyama vingine hivyo lazima apatikane mgombea
anayeuzika mwenye mvuto kwa maana ya sera kuaminika. Vyama vitengeneze utaratibu wa kuwashawishi wenye uwezo wa kuweza kuwasaidia kwenda kupambana kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Dk Loisulie.
Alisema vitendo vyovyote vinavyoenda kinyume na ustaarabu wa kufanya siasa lazima vikemewe.
Kwa upande wake, Mchambuzi wa siasa, Hamduni Marcel alisema ni lazima vyama viangalie historia ya mtu anayeomba ridhaa ya kugombea na kuangalia matakwa ya wakati ili kupata kiongozi bora atakayeweza kuwatumikia wananchi.
“Lazima wazingatie kupitisha wagombea ambao wanajua ni wazalendo wanaofanya siasa kwa kujua ni Mtanzania na huna pa kwenda zaidi ya hapa, hilo ni kubwa kuliko jambo lolote,” alisema Marcel.
Imeandikwa na Selemani Nzaro na Lidya Inda



