Vyama vyaungana uandikishaju daftari la mkazi

WAKATI zoezi la uandikishaji la wapiga kura katika daftari la mkazi kwa ajiili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ukitarajia kukamilika Jumapili hii, viongozi wa vyama vyote vya siasa mkoani Kigoma wameungana kuhamasisha wananchi kujiandikisha.

Viongozi hao wakiungana na msimamizi wa uchaguzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kisena Mabuba walitembelea mwalo wa Katonga Mjini Kigoma ambapo walifanya mkutano wa uhamasishaji.

Akizungumza katika mkutano huo wa uhamasishaji, Katibu wa CCM Wilaya Kigoma Mjini, Sadick Kadulo amewaambia wananchi hao kuwa kujiandikisha na kupiga kura kwa wananchi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndiyo msingi wa ngazi ya maendeleo.

Msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Kigoma Mjini Kisena Mabuba (kushoto) akizungumza katika zoezi la uhamasishaji wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la wakazi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa

Katibu wa Jimbo la Kigoma Mjini kutoka chama cha ACT Wazalendo, Iddi Adam amesema vyama vinaungana na serikali kuhamasisha zoezi hilo ili wananchi wote wajitokeze kujiandikisha kushiriki kwenye zoezi la uchaguzi na kwamba wanafanya hivyo bila kujali itikadi za vyama.

Akizungumza katika mkutano huo, msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini, Kisena Mabuba amesema zoezi la uandikishaji kwa sasa na upigaji kura hapo baadaye ni jambo linalowahusu watanzania wote bila kujali misingi ya vyama vyao, dini wala Kabila.

Katibu wa CCM Wilaya Kigoma Mjini Sadick Madulu akizungumza katika mkutano wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la mkazi kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Mabuba ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji amesema kuwa kutokana na hilo ndiyo maana ofisi yake imezungumza na viongozi wa vyama vyote vya siasa na kukubaliana kuendesha mikutano ya kampeni ya uhamasishaji.

Hassan Sadi Mwenyekiti wa Chama cha UDP akizungumza katika mkutano wa uhamasishaji

Habari Zifananazo

Back to top button