Vyombo vya usalama vyajipanga kumkamata Yoon Suk

KOREA KUSINI : RAIS wa Korea Kusini aliyesimamishwa kazi, Yoon Suk Yeol, anakabiliwa na jaribio jipya la kukamatwa baada ya mkuu wa timu ya uchunguzi kuahidi kwamba watafanya kila liwezekanalo kuvunja vizuizi vya kiusalama na kumkamata kiongozi huyo aliye na mashtaka mazito dhidi yake.
Mapema leo Jumatano, waandamanaji wanaomuunga mkono na wanaompinga Yoon walikusanyika karibu na makazi yake wakizozana, huku mahakama ikitoa waranti nyingine ya kumkamata rais huyo aliyeingiza nchi hiyo katika machafuko ya kisiasa mwezi uliopita kwa kutangaza kuanzisha sheria ya kijeshi.
Tangu wakati huo, Yoon amejiweka kando, akijificha katika makazi ya rais na kugoma kuitikia wito wa kwenda kuhojiwa na timu ya wachunguzi.
Mkuu wa Ofisi ya Uchunguzi wa Kesi za Ufisadi kwa Viongozi wa Vyeo vya Juu, Oh Dong-Woon, alikiri kushindwa kwa jaribio la kukamatwa Yoon Ijumaa iliyopita, baada ya mvutano mkali wa saa sita katika makazi ya rais mjini Seoul.
Mkuu huyo aliomba radhi kwa kushindwa kwa juhudi hizo na ameahidi kufanya kila liwezekanalo ili kufanikisha jaribio la kumkamata Yoon. SOMA: Yoon Suk agoma kukubali kushindwa