Waagizwa kukamilisha miradi ya maji Sep.30

Waagizwa kukamilisha miradi ya maji Sep.30

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, ameagiza kukamilishwa na kuanza kutoa huduma ya maji, miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za Uviko-19 mkoani Kagera, ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Mhandisi Kemikimba alisema miradi hiyo ilitakiwa kuwa imekamilika mwezi Juni kwa mujibu wa mikataba, hivyo kutokamilika kwa wakati inafanya wananchi kuendelea kupata adha ya maji, tofauti na malengo ya serikali.

Alitoa kauli hiyo alipokuwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya maji Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera,  alipotembelea mradi wa maji wa Buyango na kujionea hali ya utekelezaji wa mradi huo.

Advertisement

Alimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji, ili malengo ya serikali kuwafikishia wananchi maji yanafikiwa.

“Nimejionea mwenyewe hali ya utekelezaji wa mradi huu, ambao ulitakiwa kukamilika mwezi Juni, ila kutokana na changamoto, ambazo tayari tumeshazitatua, naagiza miradi yote mkoani Kagera, ukiwemo huu, ikamilishwe kabla ya Septemba 30, mwaka huu,” alisema Kemikimba.

Kwa upande wake mkandarasi, Athumani Mkono kutoka kampuni ya Advanced Engenering Company ltd, alisema sababu zilizofanya kuchelewa kwa mradi huo, ni kuchelewa kwa mabomba ambayo yananunuliwa na wizara, kuwepo miamba kwenye njia za kupitisha mabomba, hali iliyofanya kutumia muda mrefu wa kuchimba mitaro, sambamba na kuchelewa kwa fedha.

Awali kwenye taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, iliyotolewa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Misenyi, Mhandisi Andrew Kilembe, alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 575.8, utekelezaji wake umefikia asilimia 85.

/* */