Waajiri Mtwara watakiwa kuangalia haki za wafanyakazi

MTWARA; CHAMA cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) mkoani Mtwara, kimewaomba waajiri kutoka taasisi mbalimbali mkoani humo kuendelea kuangalia haki za msingi za wafanyakazi ikiwemo mkataba na masuala mengine.

Akizungumza leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, wakati wa Maadhimisho ya Mei Mwaka 2024, Katibu wa TUICO mkoani humo, Alice Chonya amesema majukumu ya chama hicho ni pamoja na kutetea, kulinda maslahi ya wafanyakazi hasa wanapokuwa kazini.

Advertisement

Amesema wanafahamu waajiri wanatoa haki na maslahi ya wafanyakazi, lakini chama hicho ni haki yao pia kuwaelekeza wafanyakazi kujua haki na maslahi yao, kutetea staha zao wanapokuwa kazini na kutoa ushauri mbalimbali.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amewataka wafanyakazi hao kama kuna changamoto na waajiri katika maeneo yao wawasilishe changamoto hizo kwa Wakuu wa Wilaya ili ziweze kushughulikiwa.

” Watumieni wakuu wa wilaya kuwasilisha changamoto zetu na waajiri wenu zitatatuliwa, msisubiri ziongezeke,”amesema Sawala.