Waajiriwa wapya 553 Takukuru wabanwe wasihame

SERIKALI imeiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) izuie waajiriwa wapya 553 katika taasisi hiyo wasihame hadi baada ya miaka mitano.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru aweke kipengele kwenye mkataba wa waajiriwa hao chenye sharti hilo.

Ametoa maelekezo hayo Jumanne Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akifunga mafunzo ya maofisa uchunguzi na wachunguzi wasaidizi wapya wanaoajiriwa na Takukuru.

Mafunzo hayo yalitolewa katika Shule ya Polisi Tanzania ili kuwajengea uwezo wa kupambana na vitendo vya rushwa.

“Ninaelekeza kwa ajira hizi 553 za Takukuru kiwekwe kipengele kinachoainisha kuwa ni lazima waitumikie Takukuru si chini ya miaka mitano bila kuhamia taasisi nyingine kwani serikali imewekeza kiasi kikubwa katika kuwapatia mafunzo na kuwaajiri, hivyo ni lazima muutumikie umma katika mapambano dhidi ya rushwa ili thamani ya fedha iliyowekezwa ionekane,” alisema Ndejembi.

Alisema ametoa maelekezo hayo ili kukomesha tabia ya baadhi ya watu kuomba kazi yoyote inayotangazwa serikalini na akiajiriwa anataka kuhamia taasisi nyingine wakati serikali imemuajiri ili kuutumikia umma wa Watanzania katika taasisi aliyopangiwa.

Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha kuichukia rushwa na kutotaka kuona maendeleo ya taifa yanakwamishwa, hivyo akaagiza waajiriwa hao wapya wa Takukuru waunge mkono kwa vitendo azma hiyo ya Rais.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni aliagiza waliohitimu mafunzo hayo kukubali kituo atakachopangiwa ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia kupambana na rushwa.

“Sitarajii kuona vimemo vya kuniomba niwabadilishie vituo vya kazi kwani wakati mnaomba ajira na wakati mnafanya usaili tuliwauliza kama mko tayari kufanya kazi popote nchini, na kila mmoja wenu alisema kuwa yuko tayari kufanya kazi sehemu yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Hamduni.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema Rais Samia ametoa ajira hizo 553 za Takukuru kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Babu aliwataka watakaopangiwa kwenye mkoa wake wafanye kazi kwa bidii na uadilifu katika kusimamia fedha za miradi ya maendeleo ambazo Rais Samia amezitoa kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button