DAR ES SALAAM: Waandishi wa habari wameaswa kufuata kanuni na maadili ya uandishi wa habari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Patrick Kipangula kwenye mkutano wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapigakura jijini Dar es Salaam.
Ameyataja baadhi ya mambo ya kuzingatia ni pamoja na kutoa elimu na taarifa sahihi za ukweli za uchaguzi, kutoa taarifa za wagombea na sera zao, kulinda faragha na utu wa mtu, masahihisho pamoja na kuhakikisha mazingira ya amani na uwazi, ili kulinda amani ya nchi.
Amewataka waandishi wa habari kutoa fursa sawaa kwa wagombea katika mchakato mzima wa uchaguzi, ili kusaidia wananchi kufanya maamzi sahihi katika kuchagua viongozi.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya mpiga kura wa INEC, Giveness Aswile amesema waandishi wanapaswa kuwa wazalendo kuhusu uchaguzi na kutenga vipindi maalumu, ili wananchi wapate elimu .