Waaswa kutoka mafichoni warekebishwe maumbile bure
DAR ES SALAAM: WANANCHI wametakiwa kuwatoa mafichoni wanawake na watoto wakike wenye changamoto ya maumbile hususani wenye majeraha makubwa ya moto, kasoro kubwa za kimwili, wahanga wa ukatili wa kijinsia na athari zitokanazo na saratani ikiwemo saratani ya matiti ili kujitokeza kupatiwa matibabu ya bure ya upasuaji na kurekebisha viungo ‘reconstruction and plastic surgery’.
Hayo yameelezwa na Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Aga Khan, Idan Njau, katika Mkutano na waandishi wa habari kutangaza programu ya pamoja kwa mwaka wa nane kati ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Aga Khan na Shirika la Kimataifa la Reconstructing Women International (RWI).
“Tusiwafiche watu hawa waliopata majanga haya, muwatoe waweze kupata huduma ya kina, ya hali ya juu na kisasa zaidi. Huduma hii ni bure, na tunakwenda kwa wale ambao wamepata matatizo makubwa sana. Tutawalipia nauli, malazi watakapofikia na baada ya matibabu tutawalipia hadi vidonda vitakapokuwa salama. Pia tutawalipia nauli za kurudi kwao watakapokuwa bukheri wa afya,” amesema Dk. Njau
“Sasa hivi programu hii inakwenda nchi nzima kutokana na uhitaji. Tutaratibu upatikanaji wa wagonjwa katika vituo vyetu vilivyopo nchi nzima lakini kituo kikuu cha matibabu ni Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.” Amesema Njau
–
Akizungumzia mikakati ya programu awamu ya 8, Afisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Sisawo Konteh amesema kati ya Novemba 28 na Desemba 02, 2023, Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imepanga kufanya pasuaji 25 za kuyarekebisha maumbile kwa wanawake na wasichana 25.
–
Akiongea kwa niaba ya RWI, Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Shule ya Matibabu ya Harvard, Andrea Pusic amesema matibabu haya yatasimamiwa na timu ya wataalamu sita kutoka Mataifa ya Norway, Canada, Uswisi na Marekani.
Kwa upande wake, Daktari wa upasuaji ‘surgeon doctor’s kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Edwin Mrema amesema programu hii pia ni fursa ya kielimu kwa kuwajenga uwezo wataalamu wa ndani.
“Tokea programu hii ianze (mwaka 2016) tumeshafanya pasuaji kwa wagonjwa 400 na wamepatikana madaktari wanane. Watano wapo shule, wanne wapo Tanzania na wawili wapo nje ya nchi (Ethiopia na Kenya) kwaajili ya Shahada ya uzamili katika ‘plastic surgery’. Amesema Mrema.
–
Naye, Daktari Mwandamizi wa Upasuaji, na Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, Athar Ali, amesema programu hiyo inalenga kurejesha utendaji wa kimwili ili kuwezesha na kuboresha maisha ya wanawake na wasichana wa Tanzania.
–
“Katika awamu saba zilizopita kati ya mwaka 2016-2022, wataalamu 16 wakiwemo madaktari wa upasuaji wa kurekebisha maumbile, madaktari wa upasuaji wa kawaida, na madaktari wanafunzi kutoka hospitali mbalimbali za umma (Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Bugando, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam) wamepata mafunzo kupitia programu hii.” Amesema Dk. Athar.