Wabunge EALA watakiwa kuendeleza mtangamano EAC

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, amewasihi wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuendeleza mtangamano ili kukuza biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Amesema suala hili ni muhimu kwani lazima kwenda pamoja katika sekta mbalimbali hususani programu za kuendeleza miundombinu inayoakisi uchumi wa kijiografia.

Aliyasema hayo jana jijini hapa katika hafla ya kuwaapisha wabunge wapya wa EALA. Alisema changamoto za ulinzi na usalama pia lazima zishughulikiwe ipasavyo ili nchi za EAC ziwe na amani.

EALA inachagua spika leo. Wabunge wa Tanzania waliochaguliwa na kuapishwa katika EALA ni Angela Kizigha, Dk Shogo Mlozi, Dk Abdullah Makame, Machano Ali, Mashaka Ngole, Ansar Kachambwa, James Millya, Dk Ngwaru Maghembe na Nadra Mohammed.

Katika hafla hiyo, pia spika wastaafu wa EALA akiwemo Abdulrahman Kinana, Martine Ngoga na Margareth Zziwa walikuwepo.

Mmoja wa wabunge kutoka Tanzania walioapa wakiongozwa na Katibu wa EALA, Alex Obarti, Millya, aliomba Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika nchi za EAC.

Millya alisema atakuwa balozi mzuri wa kuisemea Tanzania na EAC kila mkoa ili kutangaza fursa zilizopo EAC.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania kwa kuaminiwa kuwa miongoni mwa wabunge hao kutoka Tanzania na kuongeza kuwa, atahakikisha kila fursa za kibiashara anazitumia.

Habari Zifananazo

Back to top button