Wabunge: Mahitaji ya mafundi mchundo, sanifu ni makubwa

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri serikali kuendelea kufanya maboresho makubwa katikaTaasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) Chuo cha Morogoro ili kiweze kukidhi mahitaji ya mafundi mchundo na mafundi sanifu ndani ya nchini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso amesema hayo kwa niaba ya wajumbe wa kamati wakati wa majumuisho baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo moja la taaluma lenye ghorofa nne eneo la makao makuu ya taasisi hiyo mkoani Morogoro.
Kakoso alisema nchi inategemea maeneo mawili ya chuo hicho makao makuu yake pamoja na kampasi ya Mbeya ( Kiwira) kwa ajili ya kupata mafundi mchundo na mafundi sanifu licha ya kumekuwepo shughuli nyingi na kubwa za ujenzi hapa nchini kwa hivi sasa.
“ Tunaomba serikali,wizara na chuo hiki mjiandae kutoa wataalamu hasa mafundi wale ambao ni adimu zaidi ndani ya nchi yetu kwani vyuo vingi vilivyoanzishwa kipindi kile cha nyuma ambavyo vilitoa mafundi wengi hapa nchini vilipoteza mwelekeo,” amesema Kakoso.
Kakoso amesema kukosekana kwa wanataaluma hayo ni kwa sababu kila chuo kilichokuwepo kilikimbilia kwenda kutoa shahada na matokeo yake kukawa na uhaba kubwa ya mafundi mchundo na mafundi sanifu ndani ya nchi yetu.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema kutokana na sababu hiyo kumefanya miradi mingi ya ujenzi ikose watu wenye utaalamu halisi kwa vile vyuo vimetoa wataalamu wengi ambao ni wasimamizi.
“Jambo hili linadhihirisha kuwa mtu akishapata shahada atajiona yenye sasa ni mtu wa kwenda kumsimamia mtu mwingine na matokeo yake unayeenda kusimamia hayupo,” amesema Kakoso.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema kuwa jitihada zinazofanywa na serikali zimeonekana na kamati hiyo na hivyo alitumia fursa hiyo kuiomba wizara ya ujenzi kuendelea kusimamia yale ambayo wabunge wameshauri ili yaweze kuleta mafanikio makubwa.
“Kamati inapongeza Serikali kwa mradi huu muhimu, sasa niiombe wizara zinapohitajika fedha za kukamilisha mradi huu zitolewe kwa wakati ili kutoa tija inayohitajika,” amesema Kakoso.
Kakoso amesema kuwa malengo ya serikali, wizara na chuo hicho ni kuweka jitihada kubwa katika kusaidia kupata wataalam hasa mafundi mchundo na mafundi wasanifu .
“Mnajua tumeanza hapa (makao makuu Morogoro) na tunatengemea ile Kampasi ya Mbeya (Kiwira) kwa mwaka ujao mheshimiwa Naibu Waziri mfikirie kwenda kujenga jengo lingine kule…lazima Serikali na wizara tuwe na mipango endelevu itakayo tusaidia kubuni vitu vingi,” amesisitiza Kakoso.
Amesema kuwa endapo mradi huo utasimamiwa vizuri una fedha zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ,wataijengea heshima nchi ,kuijengea heshima wizara kwa kuwa asilimia kubwa ya mradi huo umetokana na msukumo na bunge .



