Wabunge mikoa ya Magharibi watembelea Bandari ya Karema

KATAVI: WABUNGE kutoka mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma wametembelea Bandari ya Karema iliyopo wilayani Tanganyika, mkoani Katavi, kushuhudia maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo pamoja na meli nne kubwa zinazojengwa kwa ajili ya kuboresha usafiri na biashara katika Ziwa Tanganyika.
Katika ziara hiyo ya pamoja, wabunge hao wamesema wameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa miundombinu, ambao unatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa mikoa ya Magharibi mwa Tanzania na kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za DR Congo, Burundi na Zambia.
Kila meli inayojengwa inatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani 2,000 za mizigo, hatua ambayo inaelezwa kuwa muhimu katika kufanikisha usafirishaji wa bidhaa kupitia Ziwa Tanganyika.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ambaye aliungana na wabunge hao katika ziara hiyo, amesema serikali inalenga kuifanya bandari ya Karema kuwa kitovu cha biashara kikanda, na kuongeza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya usafirishaji wa majini.
Mbunge wa Jimbo la Tanganyika, Selemani Kakoso, ametoa wito kwa wakandarasi kuhakikisha wanazingatia sheria za ajira na kuwashirikisha wananchi wa maeneo ya jirani katika fursa za ajira za muda na za kudumu.
Mradi wa bandari na meli katika Ziwa Tanganyika ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikilenga kufungua fursa za kiuchumi kwa maeneo ya pembezoni na kuiunganisha Tanzania na masoko ya kikanda.