Wabunge waagiza TSN, TBC walipwe madeni

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza serikali ihakikishe taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zinalipwa madeni ya muda mrefu zijiendeshe kibiashara.

Baadhi ya taasisi zilizotajwa kuwa na madeni ya muda mrefu na kushindwa kukopesheka ni Shirika la Posta, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso alisema Dar es Salaam jana kuwa ni lazima serikali isimamie madeni hayo ili mashirika hayo yakopesheke na kujiendesha kibiashara.

Kakoso alisema kuwa TTCL, Posta, TSN na TBC wana miradi mingi, lakini kutokana na madeni hawakopesheki hivyo serikali iweke mikakati ya kuwasaidia.

“Wizara iangalie namna ya kuongeza bajeti kwa TBC kwani kutokana na bajeti yao haiwezi kwenda kwenye ushindani wa soko la habari, lakini katika Chaneli ya Safari haipati chochote na ndio maana wanarudia vipindi kwa sababu hawana uwezo wa kuandaa vipindi vipya kwa kuwa hawana fedha, muone namna ya kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii,” alisema Kakoso.

Alipongeza serikali kwa ununuzi wa mtambo wa kuchapa magazeti wa TSN kwa kuwa utasaidia uchapaji wa kiwango cha juu na kuwa kitovu cha uchapishaji nchini.

Alisema mtambo huo ni wa kipekee Afrika Mashariki hivyo aliagiza TSN wajitahidi kujitangaza ili wajiendeshe kibiashara.

“Mtambo huu ni mkubwa hivyo hakikisheni mnautunza kuhakikisha mnapata masoko maeneo mbalimbali na kufanya shughuli za biashara bila kutegemea ruzuku,” alisema Kakoso.

Pia aliishauri serikali ihakikishe Mkongo wa Taifa unaosimamiwa na TTCL unajiendesha kibiashara ili kuleta mapinduzi katika sekta ya mawasiliano.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema mpango wao ni kuhakikisha madeni yote ya taasisi zilizo chini ya wizara yanalipwa.

Nape alisema TSN pekee inadai zaidi ya Sh bilioni 11 na wameanza uhakiki wa madeni yanayoweza kulipwa yalipwe na yanayoweza kugeuzwa kuwa mtaji wafanye hivyo.

Alisema mchakato wa kuzifanya taasisi hizo kujiendesha kibiashara unaendelea na ndio maana wamewapa TTCL mkongo na kituo cha data wasimamie na kujiendesha.

Pia alisema wamefanya mabadiliko ya Sheria ya Posta ili kuwafanya wajiendeshe kibiashara sanjari na kuwataka kuwa na ubia na taasisi mbalimbali.

“Tumepokea maelekezo ya Kamati ya Bunge ya kuharakisha mchakato wa taasisi hizo zijisimamie kibiashara. Kuhusu upatikanaji wa huduma za redio mipakani, tumeelekeza TTCL kushirikiana na watoa huduma za redio kuongeza kasi ya upatikanaji wa masafa ya ndani,” alisema Nape.

Habari Zifananazo

Back to top button