Wabunge wapitisha bajeti Mambo ya Nje

DODOMA; WABUNGE wamepitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mapema leo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba aliwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25 mjini Dodoma , akiomba bunge liidhinishe jumla ya Sh 241,069,232,000.

Akiwasilisha makadirio hayo ametaja vipaumbele vya wizara hiyo kuwa ni kuratibu utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ili kuchochea uwekezaji, utalii, na biashara pamoja na kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Kuendelea kuimarisha uratibu na ushirikiano wa uwili pamoja na ushiriki wa Tanzania katika jumuiya na mashirika ya kikanda na kimataifa ili kulinda maslahi ya taifa; pamoja na kustawisha diplomasia ya kisasa na kujenga uhusiano wa karibu na nchi washirika.

“Kuongeza ushawishi wa Tanzania kwa nchi nyingine katika masuala mtambuka, kwenye Jumuiya na Mashirika ya Kikanda na Kimataifa,” amesema na kutaja vipaumbele vingine ni kushiriki kwenye jitahada za kikanda na kimataifa za kudumisha amani, ulinzi na usalama.

“Kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, kuimarisha utawala bora na rasilimaliwatu pamoja na kutekeleza miradi ya ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi, makazi ya watumishi na vitega uchumi katika balozi za Tanzania na makao makuu,” amesema Waziri Makamba.

 

Habari Zifananazo

Back to top button