Wabunge wapongeza uwekezaji Bandari Mtwara

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imesema serikali ilifanya jambo la muhimu kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya Bandari ya Mtwara.

Akizungumza baada ya kamati hiyo kutemebelea bandari hiyo leo Machi 25, 2024, Mwenyekiti wa kamati hiyo Deus Sangu amesema uwekezaji huo umekuwa na tija kubwa kibiashara katika bandari hiyo.

“Jambo kubwa na la muhimu ambalo serikali ilifanya na limeleta faida kubwa ni uwekezaji wa shilingi takribani bilioni 157 katika Bandari  hii ya Mtwara, uwekezaji huo umeleta mapinduzi makubwa Sana,” amesema.

Advertisement

Akitoa taarifa ya maendeleo ya bandari hiyo, Naibu Mkurungezi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi Bandari Nchini (TPA) Mhandisi Juma Kijavara, amesema uwekezaji huo umeiwezesha bandari kuhudumia shehena tani milioni 1.1  na kuvuka lengo.

Kabla ya uwekezaji huo, bandari hiyo ilikuwa na uwezo wa kuhudumia tani 400,000 tangu ilivyojengwa mwaka 1954.

Kwa mujibu wa taarifa, kipindi cha mwaka 2022/2024 Bandari ya Mtwara ilihudumia mizigo tani 1,126,300 na kuvuka lengo la kusafirisha tani 1000,000 kwa mwaka.

Kijavara amesema bandari iliweka lengo la kusafirisha tani milioni 1.2 kufika mwaka 2025, ambapo lengo hilo limefikwa kabla ya kipindi husika.