Wabunge wasisitiza NEMC kuwa NEMA

WABUNGE wa Bunge la Tanzania wamesisitiza msimamo wao kutaka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira( NEMC) kuwa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi Mazingira (NEMA).

Msimamo huo wameutoa leo bungeni jijini Dodoma wakati wakichangia Mswada wa Marekebisho Madogo ya Sheria ya Mazingira Sura 191 kwa kuitaka serikali kuhakikisha inapeleka Mswada wa Sheria kuanzisha NEMA.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Maji na Mazingira imesema ni wakati muafaka NEMC kuwa mamlaka hasa ikizingatiwa kuwa nchi imekabiliwa na changamoto nyingi za kimazingira.

Advertisement

Akisoma taarifa ya kamati kwa niaba ya Mwenyekiti, Mbunge wa Viti Maalum( CCM) Mkoa Mtwara , Agness Hokololo ameitaka serikali kupeleka bungeni Mswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ili NEMC kuwa NEMA.

” Mhe Mwenyekiti, sisi katika kamati moja ya mambo ambayo tunayatarajia ni kupata mswada mpya wa NEMC kuwa NEMA pamoja na Uchumi wa Buluu,” amesema Mbunge Agness.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jackson Kiswaga ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kalenga amesema ni matamanio ya kamati kumpatia Rais Samia Suluhu Hassan chombo chenye nguvu( Mamlaka-NEMA) kitakachosimamia mazingira.
“Ni matamanio ya Kamati kuona tunampatia Rais chombo chenye nguvu nacho si kingine ni kuifanya NEMC kuws Mamlaka,” amesema Mbunge Kiswaga.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya amesema NEMC inahitaji kuwa na chombo madhubuti kusimamia sekta hiyo hivyo, ameshauri NEMC kupandishwa hadhi kuwa Mamlaka- NEMA.

Nae Mbunge, Profesa Shukurani Elisha amesema ni muhimu serikali kuwasilisha marekebisho makubwa ambayo yatawezesha NEMC kuwa mamlaka.

“Ni matarajio ya Kamati katika Bunge lijalo, uletwe Mswada wa Sheria kubadilisha Baraza la Taifa la Hifadhi Mazingira kuwa Mamlaka,” amesema Mbunge Profesa Elisha.

Mbunge huyo alijenga hoja ya kwanini NEMC iwe NEMA, alitaja baadhi ya changamoto ambazo NEMC inashindwa kutasimamia.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kushamiri kwa matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo ilipigwa marufuku, utupaji taka katika fukwe za bahari na maziwa, uchimbaji wa madini usiozingatia uhifadhi wa mazingira, kelele hasa wakati wa usiku katika mitaa mbalimbali, ujenzi katika vyanzo vya maji, vilima.

Mbunge huyo amesema mambo hayo na mengine, ndiyo yanayopelekea Kamati ya Kudumu ya Maji na Mazingira kutaka NEMC kuwa NEMA ili iweze kusimamia kwa ufanisi.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge Profesa Patrick Ndakidemi amesema anaunga mkono NEMC kuwa Mamlaka.

Akitoa majumuisho ya michango ya Wabunge, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais( Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Masauni ameahidi mbele ya bunge kuwa serikali itawasilisha katika bunge lijalo Mswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ambapo pamoja na mambo mengine kuipandisha hadhi NEMC kuwa Mamlaka.
Msimamo huo wa wabunge unaungwa mkono na wadau wa mazingira ambao wanataka NEMC kuwa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira nchini.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *