MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Thomas Roy Ole Sabaya amewataka wabunge wote mkoani Arusha kujifunza kwa Mbunge wa Jimbo la Longido ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa namna ya kuwaletea maendeleo wananchi na kutatua changamoto zao.
Sabaya amesema jana mara baada ya Kiruswa kusoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi cha miaka mitano aliyokuwa Mbunge mara baada ya wajumbe hao kuonyeshwa kwa video wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wa Wilaya ya Longido miradi yote iliyotekelezwa katika kipindi hicho.
Amesema Kiruswa ni Mbunge wa aina yake katika Mkoa wa Arusha asiyekuwa na makundi, mwenye heshima, hana dharau, mnyenyekevu na hana makeke hivyo wabunge wengine wanapaswa kujifunza kutoka kwake.
Mwenyekiti huyo amesema sifa alizonazo Kiruswa ndio zimemsukuma Rais Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa Naibu Waziri wa Madini na ni waziri pekee mkoani Arusha hivyo alistahili kuteuliwa kwani amemsaidia sana Rais kusukuma maendeleo Longido.
‘’Wabunge mkoani Arusha acheni makeke igeni tabia ya Kiruswa mtaisaidia kwa kiasi kikubwa CCM kufanya kazi yake kwa urahisi katika uchaguzi ujao, majivuno, makundi na dharau kwa wengine haitawasaidia,’’alisema Sabaya
Aidha mwenyekiti huyo amewataka madiwani katika kata zote 18 za Longido kuhakikisha na wao wanasoma taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Mkutano Mkuu wa Kata ili kuwaeleza wanaowaongoza shughuli walizofanya katika kipindi cha miaka mitano.
‘’Hii sio ombi ni kwa mujibu wa kanuni ya Katiba ya CCM inaeleza hivyo kutoka kwa mbunge, diwani na Rais lazima wazungumze walichokifanya katika kipindi hicho,’’alisema Sabaya.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salumu Kalli mbali na kumpa maua yake Kiruswa kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa ilani ya CCM Katika Jimbo la Longido aliwataka wanachama wa chama hicho kumpa ushirikiano mbunge kwani ndio njia pekee ya kuleta maendeleo Longido.
Kalli alisema kuna baadhi ya watu bado ni vipofu na wanajifanya hawaoni kilichofanywa na Kiruswa na Rais katika jimbo la Longido hivyo aliwaasa kuacha fitina hizo kwani hazitawasaidia kwa sasa kwa kuwa watu wote wanaona tofauti ya sasa na miaka ya nyuma katika Jimbo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Longido, Saimon Oteseu amesema mbunge na madiwani wamekuwa wakishirikiana kwa hali na mali katika kutatua changamoto za wananchi wa Jimbo la Longido na kuwaletea maendeleo na sio vinginevyo.
Amesema fedha zote zilizopelekwa Longido na Rais zimetumika kama zilivyokusudiwa kwa usimamizi madhubuti wa mbunge na madiwani katika kila kata na ndio maana wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa wameichagua CCM kwa asilimia mia moja pamoja na kwamba vingine vilijitokeza kuwani nafasi za kijiji na vitongoji.