HEKAHEKA za usajili kuelekea msimu ujao kwa timu za Simba, Yanga na Azam zimezidi kushika kasi kila upande ukipambana kupata wachezaji ambao wanaamini watawapa mafanikio msimu ujao wa 2023/24.
Ikumbukwe timu hizo msimu ujao zitapeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa, Simba na Yanga zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam FC itapigania Kombe la Shirikisho Afrika.
Ingawa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) bado halijatangaza tarehe rasmi ya dirisha la usajili kufunguliwa, lakini moto wa viongozi wa timu hizo umekuwa mkubwa zaidi ya kawaida kila upande ukitaka kuweka mitambo yake sawa kabla ya vita ya mataji kuanza.
Pamoja na sifa nyingi wanazopewa wachezaji hao kupitia kwa mawakala au mameneja wao picha za video, lakini bado inakuwa vigumu kuamini kama nyota hao wanaweza kutamba na kuleta mafanikio kama ambavyo viongozi wa timu hizo wanatarajia isipokuwa kwa wale wachezaji ambao tayari wanafahamika uwezo wao.
Kwa kuliangalia hilo makala haya inaeleza kuhusu wachezaji ambao baadhi yao wameshakamilisha taratibu za kujiunga na timu hizo, lakini swali linakuja je, watazibeba timu zao kama ilivyo ukubwa wa usajili wao?
1.Feisal Salum- Yanga kwenda Azam FC Huu ndio usajili ambao umetingisha Tanzania kuanzia dirisha dogo la msimu uliopita hadi sasa, kiungo huyo tayari amekamilisha usajili wake na Azam FC akitokea kwa mabingwa wa Bara, Yanga, uwezo aliokuwa nao haumpi shaka mtu yeyote, swali ambalo watu wanajiuliza je, kiwango alichokionesha akiwa na Yanga atakiendeleza Azam FC?
Fei Toto akiwa Yanga alipata mafanikio makubwa na kuibeba timu hiyo katika mechi ngumu ndio maana hata viongozi wa Yanga, hawakuhitaji kumpoteza mchezaji huyo, lakini Azam ni timu ambayo wamepita wachezaji wengi bora na wengi wao walipokuwa hapo walipotea kwenye soka la ushindani
- Gibril Sillah- Raja kwenda Azam FC
Hili ni ingizo jipya kwenye kikosi cha Azam FC katika eneo la ushambuliaji, Sillah amesajiliwa na Azam akitokea Raja Casablanca ya Morocco akiwa na rekodi ya kufunga mabao saba kwenye ligi ya Botola.
Kwa wasifu anaonekana mchezaji mkubwa na mzuri kwenye kufunga hasa atakapojenga ushirikiano mzuri na washambuliaji waliopo akina Prince Dube, Abdul Sopu na Idriss Mbombo lakini ujio wake unaweza kumaliza ukame wa Azam FC wa kukosa taji la ligi kuu katika misimu tisa iliyopita?
Achana na Azam FC timu ambayo imekuwa na tambo na majigambo kila dirisha kubwa linapofika lakini mambo huwa tofauti msimu unapofika katikati au mwisho, kuelekea dirisha hilo tuwaangalie Simba ambayo tayari imekaa misimu miwili bila kubeba taji lolote.
Miamba hii baada ya kutoka patupu nikama imepania kwamba msimu ujao warudishe heshima yao na hiyo inatokana na usajili ambao wamekusudia kuufanya kwenye dirisha kubwa ambalo linataraji kufunguliwa hivi karibuni.
Kuthibitisha hilo Simba imetenga bajeti ya Sh bilioni 24 kuhakikisha inasajili wachezaji wenye ubora na gharama ya juu ili kurudisha mataji yote ambayo wameporwa na watani zao Yanga msimu unaokuja.
3.William Onana-Rayon kwenda Simba
Kiungo mshambuliaji raia wa Cameroon anayeichezea klabu ya Rayon Sports ya Rwanda inaelezwa kuwa tayari ameshasaini kandarasi ya miaka miwili kuitumikia Simba msimu ujao, mchezaji huyu ukiacha rekodi yake nzuri ya ufungaji kwenye ligi ya Rwanda lakini kimo chake na mwili wake ulivyojengeka vinaonesha ni mtu sahihi lakini mahitaji ya Simba ni makubwa, swali ataweza kufikia malengo?
Ligi ya Tanzania kama inavyosemwa kuwa inashika nafasi ya tano Afrika kwa ubora ni kweli anaweza kuwa amefanya vizuri kwenye ligi ya Rwanda lakini anakuja Tanzania ligi tofauti na aliyoizoea, Yanga iliwahi kumsajili Michael Sarpong pia kutoka Rwanda lakini alichemka.
Lakini ukiachana na hayo eneo la ushambuliaji Simba bado lina watu sahihi ambao tayari wamemthibitishia kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kuwa ni bora kama Saido Ntibazonkiza na Jean Baleke, swali ni je, Onana ataweza kuwaweka benchi wawili hawa ili apate nafasi ya kuanza?
- Che Malone- Coton Sports kwenda Simba
Huyu ni mlinzi wa kati wa klabu ya Coton Sports ya Cameroon, Simba inaelezwa tayari imepeleka ofa ya kwanza kutaka kumsajili lakini imekataliwa na wameambiwa kuongeza ili kupata huduma ya mchezaji huyo, ambaye kwa sasa Azam FC nayo inasemekana wameingilia kati dili hilo.
Malone siyo mchezaji anayejulikana sana kwa mashabiki wa Simba, ingawa kwa changamoto na mapungufu ya beki wa kati anaweza kuisaidia timu hiyo kutokana na rekodi zake na uzoefu aliokuwa nao kwenye mashindano ya kimataifa katika msimu uliopita timu yake ya Coton Sports iliondoshwa kwenye ligi ya mabingwa katika hatua ya makundi.
Kama ilivyo kwa Simba, hata upande wa Yanga mpaka sasa bado haijathibitishwa mchezaji yeyote ambaye amesajili kwa ajili ya msimu ujao ukiacha Kocha Mkuu Miguel Angel Gamondi ingawa tayari kuna majina mengi ya wachezaji wanatajwa kumalizana na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.
5.Jonas Mkude- Simba kwenda Yanga
Lejendari wa Simba lakini msimu mbaya uliombatana na majeruhi umejikuta ukimwondoa kwenye kikosi cha Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na sasa anatajwa kutua kwenye viunga vya Jangwani msimu ujao akikabidhiwa jezi namba sita ile iliyoachwa na Fei Toto.
Bado haijajulikana kama kweli mchezaji huyo amesaini Yanga lakini maswali ni mengi kwa mashabiki wa timu hiyo kwamba anaweza kuwa mtu sahihi katika kikosi chao ambacho kina malengo ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu unaokuja? Ni suala la kusubiri na kuona.
- Mohammed ZoungranaAsec Mimosas kwenda Yanga
Nyota huyu kutoka miamba ya soka Asec Mimosas ni mchezaji anayecheza eneo la kiungo mkabaji, ameonesha uwezo mkubwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na aliisaidia timu hiyo kufika hatua ya nusu fainali kabla ya kutolewa na USM Alger.
Yanga inataja kumalizana na mchezaji huyo na kama kweli mwamba huyo atatua Jangwani anaonekana kwenda kumaliza ufalme wa Yannick Bangala ambaye msimu uliopita kwa kiasi fulani hakuonekana kuwa fiti kwa asilimia 100 ingawa bado mchezaji huyo naye itahitaji kuzoea mazingira
Comments are closed.