Wachimbaji wadogo mambo safi sekta ya madini

MBEYA: Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo kuhakikisha wanapata mitaji, leseni na matumizi ya teknolojia katika shughuli za uchimbaji wa madini na kuwezesha kukusanya Sh bilioni 33.4 ndani ya mwaka mmoja.

Hayo yamesemwa na Afisa Madini Mkazi Chunya, Mhandisi Laurent Mayala wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwatembelea wachimbaji wadogo katika eneo la Itumbi.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais  Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo kwa kutoa vifaa vya kisasa ambapo imesaidia  hivi sasa kuchimba madini kwa uhakika,”amesema Mayala na kuongeza

” jitihada hizo zimechangia kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli ya Serikali hadi kufikia Sh bilioni 33 kutoka Sh bilioni 30.4 ikiwa ni lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024,” amesema

Aidha Mayala amesema serikali inaendelea kuhamasisha mabenki kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wachimbaji wadogo ili kuweza kutatua changamoto ya mitaji yao.

Kwa upade wake mchimbaji mdogo wa kampuni ya Achimwene Bussiness Group Company Limited, Heneriko Maganga amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka mazingira wezeshi ikiwemo bei nzuri sokoni ili wachimbaji wadogo waweze kunufaika zaidi.

Amesema wataendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuendelea kutoa ajira kwa vijana na kurudisha faida kwa kile kinachopatikana katika vijiji vinavyozunguka migodi.

“Serikali imerahisisha vitu vingi ikiwemo kuhakikisha bei ya dhahabu sokoni zinakuwa juu ili wachimbaji wadogo wanufaike. Tumeendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kurudisha faida kwa jamii ikiwemo kununua kompyuta katika Shule ya Sekondari ya Matundasi, kutoa misaada kwa wasiojiweza  na kushiriki katika ujenzi wa Sekondari ya Masache,”amesema Maganga

Naye mchimbaji mdogo Hamad Shaban ameiomba Serikali kutilia mkazo suala la wachimbaji wadogo kutumia leseni zao kama dhamana ya kupata mikopo ili kukabiliana na chagamoto ya mitaji.

 

Habari Zifananazo

Back to top button