WADAU wa maendeleo wameombwa kuendelea kusaidia sekta ya kilimo nchini Tanzania, hasa kwa kundi la vijana na wanawake ili kuhakikisha wanaleta mchango katika sekta hiyo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban ametoa ombi hilo wakati akiongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano kujadili fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Kilimo na namna ya kutafuta rasilimali fedha za kukabiliana na uhimilivu wa mabadiliko ya Tabianchi.
Mkutano huo umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) unaoendelea mji mkuu wa Azerbaijan, Baku na kuandaliwa na Wizara ya Kilimo na Shirika la Care International.
Naibu Katibu Mkuu Amina amesema upatikanaji wa ufadhili endelevu na wa muda mrefu bado ni changamoto inayoendelea kwa nchi zinazoendelea hivyo ni wakati muafaka kwa wadau kusaidia katika sekta hiyo muhimu ili kupata rasilimali fedha za kutosha ili kuleta mageuzi.
SOMA: COP29 wainufaisha Tanzania hifadhi ya mazingira
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Amina ameshukuru Serikali ya Norway kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika sekta ya kilimo kinachohimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amebainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wazi ajenda na vipaumbele vya kuleta mabadiliko katika kilimo kwa lengo la kuongeza ualishaji wa mazao.
Amefafanua kuwa mikakati na sera zinaeleza kuwa ili kukuza ujuzi kwa wakulima inapaswa kutoa motisha kwa ushiriki wa sekta binafsi, kuimarisha minyororo ya thamani na shughuli za uzalishaji, kuhakikisha usalama wa chakula na uwekezaji wa miundombinu.
“Tanzania imejikita katika kuhakikisha usalama wa chakula huku ikijenga mifumo jumuishi zaidi, endelevu, yenye lishe na ustahimilivu. Katika COP 29 hata tunapoangazia ajenda tofauti, bado tunahimiza washirika tofauti kuendeleza mifumo ya chakula na hatua za hali ya hewa katika muktadha wao wa kipekee,” amesema.