Mkutano wa 29 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) umeendelea kuiletea manufaa Tanzania hususan katika hifadhi ya mazingira.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga amesema hayo wakati akizungumza mara baada ya kutembelea banda la Tanzania katika mkutano huo unaofanyika mji mkuu wa Azerbaijan, Baku.
Amesema kuwa katika kushiriki kwake amepata wasaa wa kukutana na wadau mbalimbali ambao wameonesha nia ya kuwekeza katika nishati safi, ajenda ambayo inahimizwa na Serikali chini ya kinara wa mazingira, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Hapa Baku tukiwa wanamazingira tumekutana na wawekezaji mbalimbali ambao wako wameona ni wakati sahihi wa kushirikiana nasi katika ajenda ya kulinda mazingira ikiwemo umeme jua na upepo, miradi ambayo itasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
SOMA: Dk Mpango kumwakilisha Rais Samia mkutano COP29
Kiswaga amesema pia mkutano huo umewakutanisha wawekezaji wenye nia ya kushirikiana na Tanzania katika biashara ya kaboni ambayo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais tayari imeandaa kanuni na mwongozo wake katika usimamizi wake, kwa lengo la kuinufaisha jamii.
Ameongeza kuwa, Mkutano wa COP29 umewezesha kukutana na wadau wa maendeleo ambao wameonesha dhamira yao katika kushirikiana na nchi katika teknolojia bora itakayochochea kilimo endelevu.
“Mikutano hii ya COP ni muhimu sana kwani inatuunganisha na dunia ndio kwani sisi kama nchi tunapata fursa nyingi ambazo tunakuwa hatukuweza kuzitambua, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla iendelee kushiriki na kwa manufaa ya taifa letu,” amesema Kiswaga ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga.
Hata hivyo, ameshauri kuwa Tanzania iendelee kushiriki mikutano mingine baada ya kumalizika kwa Mkutano wa COP29 akisema hatua hiyo itawapa muda zaidi wajumbe kukutana na wadau kutoka mataifa mbalimbali kwa ajili ya kutafuta fursa.