MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango anatarajia kuondoka leo Novemba 08 kuelekea Baku, Azerbaijan, kumwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29), unaotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 11 hadi 22.
Taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais iliyotolewa jijini Dodoma imesema akiwa Azerbaijan, Dk Mpango anatarajiwa kuhutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa COP-29 ambapo ataeleza msimamo na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
SOMA: Dk Mpango kuongoza ujumbe mkutano COP29
Aidha, Makamu wa Rais atashiriki mikutano ya pembezoni ikiwa ni pamoja na mkutano utakaojadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, fursa za nishati safi ya kupikia na biashara ya kaboni.
Pia, atashiriki kwenye mkutano utakaojadili namna ya kuongeza uwekezaji kwenye uchumi wa buluu katika maeneo ya bahari na maziwa makuu, kama hatua ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Sambamba na ushiriki katika mkutano wa COP 29, Makamu wa Rais anatarajiwa kufanya mikutano ya uwili na Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na viongozi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoshiriki mkutano huo ili kujadili fursa mbalimbali za maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Katika mkutano huo, Makamu wa Rais ameambatana na Viongozi pamoja na Wataalamu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.