Wadau kanda ya ziwa wataka maboresho sheria utoaji mimba

Baadhi ya wahanga wa utoaji mimba usio salama na madaktari wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wameshauri kulegezwa kwa masharti ya sheria inayozuia utoaji mimba ili kuruhusu wasichana au wanawake wanaopata mimba kwa njia za ukatili ikiwemo kubakwa wazitoe.

Sheria za Tanzania zinaeleza kuwa utoaji mimba ni kosa la jinai lakini inaruhusiwa pale tu inapoonekana ujauzito unahatarisha afya au maisha ya mama.

Mmoja wa wahanga hao, mkazi wa Buzuruga mkoani Mwanza aliyejitambulisha kwa jina la Ester John anasema yeye ni mmoja wa wanawake waliopoteza ndoto zao za maisha baada ya kubakwa na kupata ujauzito.

“Nilikuwa na miaka 16 tu nilipokutana na changamoto hiyo. Na katika hili nimekuwa muwazi na nitaendelea kuwa hivyo ili kusaidia kuwanusuru mabinti wengi wanaopata mimba kwa njia za kutatanisha,” anasema.

Bila kuficha Ester anasema alipata ujauzito baada ya kubakwa na ndugu wa damu aliyewatembelea nyumbani kwao wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

“Baada ya kupima na kubaini kuwa nimepata ujauzito  nilikimbilia Sengerema kwa ajili ya kutoa mimba hiyo, nilipofika hospitali nilinyimwa huduma kwa kile nilichoelezwa ni kosa kisheria,” anasema.

Baada ya kukataliwa, anasema ndipo alipoamua kutoa mimba hiyo kwa kutumia dawa za kienyeji kwa sababu haikuwa kwa ridhaa yake na mbaya zaidi aliyemsababishia ni ndugu yake wa damu.

“Nakumbuka nilipoteza damu nyingi sana na nilikuwa katika hali mbaya ya kupoteza maisha kabla ya kukubali nipelekwe hospitalini ambako nikiri nilipata matibabu bora ingawa nilitolewa mfuko wa uzazi kwa sababu ulikuwa umeoza,” Ester alieleza kwa uchungu.

Ester ambaye alikuwa mwanafunzi wa sekondari wakati huo anasema kama sheria ingeruhusu wanaopata mimba katika mazingira hayo watoe, huenda asingetumia dawa za kienyeji na mfuko wake wa uzazi usingeoza na kuharibika.

Binti mwingine, Amina Ismail wa jijini Mwanza pia anasema akiwa na miaka 17 alipata mimba baada ya kubakwa na mwendesha bodaboda aliyekuwa akimpeleka shuleni kila siku.

“Nashauri serikali ianze kutoa huduma ya utoaji wa mimba kwa wale wanaopata ujauzito katika mazingira kama niliyokutana nayo,” anasema.

Kwa upande wake Elizabeth Masanja kutoka Kahama Mkoani Shinyanga anasema yeye alipata ujauzito baada ya kubakwa na mwanafunzi mwenzake ambaye alimlazimisha kufanya tendo la ndoa bila ridhaa yake.

Kwa upande wao, baadhi ya Madaktari kutoka Kanda ya Ziwa walisema wanawake watatu kati ya watano wanaolazwa hospitalini kwa matatizo ya utoaji mimba usio salama ni wale wenye umri chini ya miaka 20.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Buzuruga cha jijini Mwanza, Dk Mahube Richard anasema kituo chao kimekuwa kikipokea wasichana na wanawake wanaolazwa kutokana na matatizo yanayohusiana na utoaji wa mimba.

Dk Mahube ametoa wito kwa serikali kuangalia uwezekano wa kutoa huduma ya utoaji wa mimba kwa wasichana au wanawake waliobakwa ili kupunguza changamoto vikiwemo vifo zinazotokana na utoaji wa mimba usio salama.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Nyankumbu mkoani Geita, Dk Irene Temba anasema kuongezeka kwa matukio ya ubakaji na mimba zisizotarajiwa kunaongeza haja kwa wanawake wanaopatwa na changamoto hiyo kupewa fursa ya kutoa mimba hizo katika mazingira salama kwenye vituo vya afya.

“Kwasasa utoaji mimba unaruhusiwa kisheria katika mazingira ya kuokoa maisha ya mwanamke na si vinginevyo,” Dk Irene anasema.

Naye, Mkurugenzi wa Kanda wa Mtandao wa Kimataifa wa Wanawake wa Haki za Uzazi Afrika (WGNRR AFRICA), Nondo Ejano anasema:

“Utoaji mimba usio salama unachangia hadi asilimia 19 ya vifo vya uzazi nchini Tanzania huku huduma ya afya kwa ajili ya kudhibiti matatizo ya utoaji mimba usio salama ukiigharimu serikali fedha nyingi.

Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2022, iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na idadi ya watu na afya ya uzazi, (UNFPA) inasema karibu nusu ya mimba zote, ambazo ni jumla ya milioni 121 kila mwaka duniani kote, hazikutarajiwa.

Ripoti hiyo iliyopewa jina: “Kuona Yasiyoonekana: Kuchukua hatua katika janga lililopuuzwa la mimba zisizotarajiwa,” : inaonesha idadi kubwa ya mimba zisizotarajiwa ni matokeo ya kushindwa kutetea haki za msingi za wanawake na wasichana, duniani kote.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani (WHO) mwaka 2022 lilitoa mwongozo wake kuhusu huduma ya utoaji mimba kwa lengo la kulinda afya ya wanawake na wasichana na kusaidia kuzuia zaidi ya visa milioni 25 vya utoaji mimba usio salama ambao hivi sasa unafanyika kila mwaka.

Habari Zifananazo

Back to top button