Mitaala ya elimu itoe kipaumbele mafunzo kwa vitendo

WADAU wa elimu nchini wameshauri serikali iboreshe mitaala ya masomo nchini itoe kipaumbele kwenye mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu ili iwaandae kujitegemea na kuona fursa mbalimbali badala ya kusubiri kuajiriwa.

Ushauri huo umetolewa na Mwalimu Ahmed Salim ambaye ni mkuu wa msafara wa ziara ya wanafunzi 30 wa Shule ya Sekondari Imperial ya Chalinze,Pwani walioondoka nchini juzi kwenda Misri na Israel kwa ajili ya kujifunza kilimo biashara na ufugaji wenye tija kama sehemu ya mafunzo ya vitendo.

Akizungumzia ziara hiyo kwa wanafunzi wa sekondari, Salim alisema kutokana na mabadiliko ya teknolojia na maendeleo duniani, ni lazima elimu itolewayo kwa wanafunzi iendane na mahitaji ya dunia, hivyo ziara hiyo ni fursa kwa wanafunzi hao kujifunza na kurudisha maarifa nyumbani.

“Tunatengeneza kizazi cha vijana kinachotambua fursa zilizopo nchini na jinsi ya kuzichngamkia, badala ya kusubiri wamalize chuo wasubiri kuajiriwa, hapa tunawaandaa waanze tangu wadogo alafu wajifunze kwa vitendo na kuchukua hatua,”alisema Salim.

Alisema kilimo na ufugaji ni moja ya masomo wanayofundishwa wanafunzi hayo hivyo katika kupata elimu zaidi ya vitendo wameandaa ziara hiyo ya mafunzo nchini Misri na Israel ambapo wanafunzi hao 30 wa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita watajifunza katika ziara hiyo ya siku 10 na kurudi na maarifa.

“Tunataka mwanafunzi,kijana apate elimu ya vitendo baada ya kupata ile ya nadharia darasani hii inawajengea uwezo waweze kujitegemea na kuwa viongozi wa kesho,”alisema Salim.

Akizungumzia ziara hiyo, mmoja wa wanafunzi hao, Elizabeth Mwilongo alisema wanafundishwa na kuhamasishwa kuona fursa mbalimbali katika sekta ya kilimo na ufugaji na nyingine shuleni hivyo ziara hiyo inakwenda kuwa tija kwao kwa sababu watajifunza zaidi kilimo biashara na ufugaji wa kisasa katika mnyororo wa thamani.

“Tunategemea kurudi na ujuzi na maarifa ili kusaidia nchi yetu katika sekta mbalimbali kama kilimo na ufugaji,hii inatusaidia kuwa na mawazo mapana kuona fursa na kuzichangamkia badala ya kusoma tu kwa lengo la kuajiriwa, sisi tunataka tupate maarifa tujiajiri tuinue uchumi wa taifa letu,”alisema Elizabeth.

Mzazi wa mwanafunzi anayesoma shule hiyo, Maximillian Msuya alisema utaratibu huo wa kuwa na ziara za kimasomo nje na hata ndani ya nchi ni mzuri unawasaidia wanafunzo kupanua mawazo na kujifunza kwa vitendo na hiyo inasaidia kuondoa dhana ya utegemezi akilini mwao.

Mzazi nwingine,Gilbert Mwilongo alisema wanafarijika wanapoona watoto wao wanapata nafasi ya kujifunza maarifa ya maendeleo wakiwa na umri mdogo hivyo hata wakiendelea vyuoni wanakuwa na ufahamu wa kufanya uamuzi na kuendeleza sekta mbalimbali nchini kwa tija.

Imperial ni shule iliyoanzishwa kwa malengo ya kutengeneza vijana wa kuendana na karne ya 21 ambayo inawajenga watoto wawe viongozi,wajiajiri wasisubiri ajira, wawe na ujuzi na maarifa ya kupambanua mambo na kuongoza wengine.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button