NAIBU Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa ameutaka ujumbe wadau sekta ya madini wanaotarajia kuelekea nchini China kuhakikisha safari hiyo inakuwa yenye tija kwa kuleta wawekezaji, kupata vifaa vya kisasa na kuongeza uzalishaji madini nchini.
Ujumbe wa watu 100 wadau wa sekta hiyo unaotarajia kuelekea China ni wachimbaji wadogo, wachimbaji wa kati, wafanyabiashara ya madini na watoa huduma migodoni.
Akizungumza Agosti 11, 2023 katika hafla ya kuuaga ujumbe huo jijini Dar es Salaam, Dk Kiruswa alisema Ubalozi wa China, na Kampuni ya Touchbroad ya kutoka nchini humo, imeandaa ziara ya wachimbaji kutoka Tanzania ili kuwawezesha kukutana na kukutana na wawekezaji wa sekta hiyo nchini China.
Amefafanua kuwa, lengo ni kutembelea viwanda vya kutengenezea mitambo na vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji wa madini na kupata uzoefu na wafanyabiashara wa madini wa China.
“Niwaombe kila mmoja wenu akiwa China ahakikishe anatimiza malengo yake kadri anavyoweza ili ujuzi mtakaoupata uje kuwasaidia kuboresha biashara zenu na kuongeza tija”. alisema Dk Kiruswa.
Aidha, Dk Kiruswa amezimwagia sifa taasisi za fedha kwa kuendelea kuwasaidia wachimbaji wa wafanyabiashara katika kuhakikisha wanapata mikopo kwa kuwa karibu na wafanyabiashara wa madini.
Sambamba na hilo, amewataka kuangalia uwezekano wa kupunguza riba ili kupata wateja wengi na kuruhusu wachimbaji wadogo kupata mikopo yenye riba nafuu.
Akizungumzia safari hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amewataka wachimbaji hao kutumia ziara hiyo kujifunza na kupata uzoefu.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini, (FEMATA) John Bina amesema ziara hiyo itafungua milango kuvutia wawekezaji wengi kwakuwa Tanzania ina sera nzuri katika uwekezaji.
Viongozi wengine waliohudhuria halfa hiyo ni Katibu Mkuu, Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali, Mbunge Viti Maalum Iringa, Rita Kabadi, Mkurugenzi Mtendaji, Shirika la Madini (STAMICO) Dk Venence Mwasse, Mjumbe Bodi ya Stamico na Lucas Seleli.
Comments are closed.