WADAU wa masuala ya kidigitali nchini wamemuoamba Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Selemani Jafo kuanza kuangalia sekta hiyo hasa upande wa usafirishaji fedha kidigitali yenye lengo la kuleta mabadiliko na kujenga jamii jumuishi kwa maendeleo endelevu.
Akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Viwanda na Biashara na viongozi wa vyama vya biashara Tanzania ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Meneja Mikakati wa Kampuni ya Airpay Tanzania, Mihayo Wilmore amesema ni muhimu serikali kuanza kuangalia upande mwingine wa ufanyaji biashara hasa katika sekta hiyo ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya mtandaoni.
Amesema usafirishaji fedha kwa mtandao kuna changamoto ya kutotambulika kama wafanyabiashara bali mafundi.
Soma:TSN kujiimarisha kidijiti, mauzo kuongezwa 30%
Wilmore amesema changamoto nyingine ni kutakiwa kufungua kampuni yenye ofisi kwenye Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ilihali hawahitaji kuwa na ofisi ili wafanye biashara.
Amesema kutokana na vikwazo mbalimbali soko hilo la biashara mitandaoni limekuwa chini ukilinganisha na nchi zingine za Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.
“Biashara za mitandaoni kwa takwimu zilizopo mwaka jana Kenya waliingiza Dola za Marekani milioni 244 huku Tanzania ikiingiza Dola za Marekani milioni tisa tu,”
“Tanzania tumepakana na nchi saba na nchi zote zinahudumiwa na bandari yetu ya Dar es Saalam lakini biashara ya fedha mtandaoni tupo chini kuliko wenzetu ambao wamepakana na nchi moja tu,” amesema Wilmore.
Amesema kampuni hiyo kwa sasa ipo katika nchi nne ambazo ni Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Ghana.
Miongoni mwa kero nyingine zilizoainishwa na wadau wengine kutoka kila sekta ni suala la kodi na tozo mbalimbali ambazo zimekuwa changamoto inayowakabili na kuwarudisha nyuma.
Hata hivyo, Dk Jafo ameahidi kuwa mtetezi wa kwanza kufanya mazingira ya uwekezaji kwenye biashara na viwanda akisema hamu yake ni kodi kulipwa inavyostahili.
Waziri Jafo ameagiza kupata taarifa ya kila sekta na maeneo wanayotaka yafanyiwe kazi ili kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini.
Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kumuandalia ratiba ya kila sekta ili akutane nao akiwa na Waziri wa sekta husika lengo likiwa ni kutatua kero zinazowakumba wafanyabiashara.
Amesema Tanzania ina fursa kubwa ya biashara katika nyanja mbalimbali na kama kuna vikwazo ijulikane nini cha kufanya ili mapato ya nchi yaongezeke.