Wadau wa korosho wapewa somo wadudu waharibifu

MTWARA; WADAU mbalimbali wanaohusika na usambazaji wa pembejeo za korosho kwa wakulima wa zao hilo nchini wametakiwa kuzipa kipaumbele dawa za sumu, ili kudhibiti magonjwa yanayotokana na wadudu waharibifu wa mikorosho.

Hayo yamejiri wakati wa mkutano mkuu wa nne wa mradi wa pamoja wa vyama vikuu vya ushirika wa korosho mwaka 20225/2026 uliyofanyika leo Julai 21, 2025 katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

Mkutano huo umekutanisha wadau kutoka mikoa minne inayolima korosho nchini ikiwemo Pwani, Ruvuma, Lindi pamoja na Mtwara ulioandaliwa na mradi huo wa pamoja wa vyama vikuu vya ushirika wa korosho (KCJE).

Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile amesema zipo hitilafu ambazo ameziona huko nyuma, hivyo ni muhimu wakazisema.

”Pembejeo zote ni muhimu lakini kuna zinazohitajika kutangulia, dawa za sumu kwa wakulima wa korosho zinatakiwa ziwe za mwanzo sasa tunawajazia masalfa, sumu zinachelewa kwanza kunatakiwa kudhibitiwe magonjwa yale ya wadudu,”amesisitiza Mwanjile.

Amewataka wazabuni wanaopewa kazi hiyo kwanza watangulize kuleta dawa hizo za sumu, kwani zikichelewa wanauchelewesha mkorosho kuleta matunda sahihi.

Mwenyekiti wa Wasafirishaji wa Pembejeo ikiwemo salfa za unga na viuatilifu au dawa za maji, Baisa Baisa ametoa ushauri kwa wasafirishaji wenzake kuwa, wanapopanga kusafirisha dawa za unga basi wasafirishe zote kwa pamoja za unga na za maji ili kupunguza baadhi ya changamoto wanazokutana nazo.

Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Francis Alfred amesisitiza suala la kuendeleza ushirikiano baina yao kwa sababu KCJE ni chombo muhimu katika kukuza uchumi wa zao hilo, pia anapenda kukiona chama hicho kinakuwa chenye nguvu kuliko chama kingine nchini.

Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mtwara, Nanjiva Nzunda amewataka wadau hao kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anatekeleza majukumu hayo, ili wakulima  kupata pembejeo hizo kwa wakati huku akisisitiza suala la kuendelea kushirikiana na serikali ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button