WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepokea vifaa saidizi vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na kuvikabidhi kwa shule za Sekondari Pugu, Jangwani pamoja na shule ya Sekondari Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salam wakati wa zoezi la uzinduzi na ugawaji wa vifaa hivyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe amesema wamepokea vitimwendo zaidi ya 100, na vifaa vingine kama vile, kompyuta, vishikwambi na mashine ya kufulia.
Aidha Prof. Mdoe ameeleza kuwa kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya kujifunzia kwa watoto ambao wanamahitaji maalumu ambao ni zaidi ya 92,000 wanaopatikana nchini ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni zaidi ya 30,000.
“Serikali huwa tunatenga bajeti tunanunua vifaa kama hivyo, kwa mwaka wa fedha uliopita tumegawa vitimwendo zaidi ya 530, lakini tumegawa vitabu vya nukta nundu vya maandishi makubwa, tumegawa vifaa vya kusaidia kusikia na pia tunatenga bajeti lakini haitoshelezi, hivyo basi tunawaalika wadau kujitokeza ili kuongeza nguvu kwa michango yenu kwa ajili ya kuwainua watoto wenye ulemavu kupata elimu bila kuliacha kundi hili nyuma.
“Sera yetu ya mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 linasema kwanza tusimuache mtoto nyumbani, kila mtoto apate elimu,inazungumzia pia suala la elimu jumuishi ambayo ni pamoja na kuhusisha wadau mbalimbali kwenye kutoa hiyo elimu, nawatia moyo wadau wengine waendelee kujitokeza,” amesema.
Vilevile ametoa wito kwa wazazi kutoficha watoto wenye ulemavu nyumbani kwa ajili ya kuwapatia fursa ya kusoma ambapo elimu atakayopewa itamjengea uwezo wa kujitegemea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala Maalumu Tamisemi, Ernest Hinju amesema kuna zaidi ya shule 20,000 zinazopokea watoto wenye mahitaji maalumu ambapo lengo lao ni kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata fursa sawa kama watoto wengine.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Juma Boniphace ameshukuru kuletewa vifaa hivyo katika shule yake ambapo amesema jambo hilo linakwenda kuwaboreshea mazingira watoto wenye mahitaji maalumu.