Wadau waomba iwekwe ruzuku vifaa vya hedhi

MTWARA: WADAU mbalimbali mkoani Mtwara wameiomba serikali kuendelea kuweka juhudi na ruzuku zinazohusiana na kutoa bure vifaa vya hedhi salama.
Vifaa hivyo ni taulo za kike na vingine ili kuwarahisisha wasichana na wanawake nchini upatikanaji wa vifaa hivyo.
Hayo yamejiri wakati wa maadhimisha ya Siku ya Hedhi Salama Duniani mwaka 2025 ambayo huadhimishwa kila mwaka Mei 28 kwa kuwa inawakilisha wastani wa siku za mzunguko wa hedhi kwa wanawake wengi ambao mara niyingi huwa ni siku 28.
SOMA ZAIDI: Taarifa zisizo sahihi afya ya uzazi zinagharimu vijana
Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii mkoani Mtwara (FAWOPA) kwa kushirikiana na Aga khan Foundation na serikali ya Canada.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Umoja ‘B’ iliyopo mbawala Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Fatuma Mbeha amesema serikali ione namna ya kusaidia kuondoka kodi au kupunguza ili watoto wa kike wapate vifaa hiyo kwa urahisi.
‘’Naiomba serikali isaidie katika hili ili watoto waweze kuzipata kwa urahisi kwani tunapata shida hata kwa kiasi kidogo tunachoweza kuwapa watoto hakitoshelezi kutokana na idadi ya wanafunzi waliyopo shuleni na tuna watoto wa kike 121,” amesema Mbeha.

Mkurugenzi wa Shirika hilo la FAWOPA Baltazar Komba ameyataja baadhi ya malengo ya siku hiyo ikiwemo kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi wa hedhi.
Pia kuvunja unyanyapaa na miiko inayohusiana na hedhi katika jamii, kuhamasisha serikali na mashirika kuweka sera na miundombinu rafiki kwa afya ya hedhi na kusaidia wasichana na wanawake kutopata vikwazo vya kushiriki kikamilifu katika shule, kazi, maisha ya kijamii wakati wa hedhi.
Ofisa Ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, Saumu Omary ametoa rai kwa jamii kuwa, suala la malezi ya mtoto wa kike ni jukumu la baba na mama hivyo mtoto huyo anapoingia katika balehe washirikishane kile kinachotakiwa kufanyika ikiwemo kutenga bajeti ya taulo za kike kwa ajili ya mtoto huyo.
Mwanafunzi wa darasa la sita kutoka shule ya msingi shangani, Angella Raphael amewaomba wazazi kuhakikisha watoto hao wanapata hedhi salama kwa sababu baadhi yao wanapata changamoto ya kupata hedhi salama, wanatumia siponji na vitambaa vichafu hali inayohatarisha afya zao.



