Wadhibiti ubora wanolewa usimamizi wenye tija shuleni

PWANI: Wathibiti ubora wa shule 160 kutoka mikoa ya Mtwara, Pwani, Kilimanjaro, Dodoma na Tanga wamehitimisha mafunzo ya siku tatu ya uongozi, usimamizi wa shule na utawala bora katika elimu, yaliyofanyika kuanzia Novemba 26 hadi 28, 2026, katika Chuo cha Uongozi wa Elimu (ADEM), Bagamoyo.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea washiriki weledi na umahiri katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa kuimarisha usimamizi wa shule, utawala bora na utoaji wa huduma za elimu zenye tija.

Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Uthibiti Ubora, Dkt. Ephraim Simbeye, Mkurugenzi Msaidizi wa Uthibiti Ubora kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Edward Wawa, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuongeza weledi, ubora na tija katika utekelezaji wa majukumu ya wathibiti ubora.

Wawa amesema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka, huku akiwataka washiriki kuzingatia uadilifu, ukweli na ushahidi katika taarifa wanazokusanya na ushauri wanaoutoa ili kulinda uaminifu wa mfumo wa uthibiti ubora wa elimu.

“Ni lazima muwe waadilifu; taarifa mnazokusanya na ushauri mnaoutoa uwe wa kweli, wa haki na unaotokana na ushahidi ili mfumo wetu uendelee kuaminika. Tusikome kujifunza mambo mapya, tutumie teknolojia na tushirikiane kwa karibu na walimu, uongozi wa shule, wanafunzi, wazazi na wadau wote wa elimu,” amesema Wawa.

Aidha, amesisitiza kuwa mafanikio ya kazi ya wathibiti ubora yanapaswa kupimwa kwa matokeo yanayopatikana katika mazingira ya kujifunza na ufundishaji, akiwataka kuhakikisha juhudi zao zinamsaidia mwanafunzi kupata elimu bora na kufikia malengo yake.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, amesema katika mafunzo hayo washiriki wamejengewa umahiri katika maeneo mbalimbali ikiwemo uongozi, usimamizi na utawala wa shule, utawala bora katika elimu, itifaki, usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Shule na ubora wa utekelezaji wa mtaala.

Amesema pia washiriki wamepatiwa ujuzi kuhusu ustawi na usalama wa walimu na wanafunzi, utafutaji na usimamizi wa rasilimali za shule pamoja na vigezo vya upimaji wa ubora shuleni.

Naye Mwenyekiti wa Washiriki, Mwl. Albert Mtalemwa, ameishukuru Serikali kwa kuwajengea uwezo, akiahidi kuwa washiriki watatumia maarifa waliyopata kwa vitendo ili kuhakikisha uwekezaji uliofanyika katika mafunzo hayo unaleta matokeo na kuchangia kuinua ubora wa elimu nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button