Waenda kwa miguu wana mtihani barabarani Dar
UKIWA mjini na hasa Dar es Salaam, chunga usijekukatishwa maisha
unapotembea barabarani.
Maana baadhi ya madereva, waendesha pikipiki, maguta na hata baiskeli, wamegeuka kuwa ‘wamiliki’ wa barabara wasiojali wala kuheshimu waenda kwa miguu.
Utathibitisha hili kwenye maeneo maalumu ya vivuko vya waenda kwa miguu ambako hushuhudiwa ukiukaji wa sheria za barabarani.
Pamoja na kwamba waenda kwa miguu pia wanatakiwa kuzingatia kanuni za kutumia vivuko, lakini kwa kiwango kikubwa wenye vyombo vya moto wamekuwa kero.
Ni bayana kwamba hata waenda kwa miguu hutakiwa kufuata taratibu na kanuni kwa maana ya kusimama, kuhakikisha magari yote yamesimama kabla ya kuingia kwenye kivuko cha pundamilia.
Mwenda kwa miguu anatakiwa kuchukua tahadhari kwa maana ya kuangalia mwendokasi wa gari kabla ya kuamua kuvuka. Maana kuwapo kivuko hakumpi ruhusa mwenda kwa miguu kuvuka holela.
Ingawa wapo baadhi ya waenda kwa miguu wasiozingatia tahadhari, kwa upande wa madereva,
wengi wamekuwa wakiukaji wa sheria ya usalama barabarani inayowataka kusimama au kupunguza mwendo mahali popote ambapo alama hiyo itakuwa imewekwa.
Inawezekana dereva mmoja akazingatia kusimama kupisha waenda kwa miguu, lakini bado
waenda kwa miguu wakavuka kwa wasiwasi wakihofu waendesha pikipiki na bajaji (bodaboda) ambao
huendesha watakavyo.
Bodaboda ni kundi la watumia barabara lililogeuka kuwa juu ya sheria za usalama barabarani kwani
ni nadra kukamatwa ikilinganishwa na vyombo vingine vya moto!
Sheria inaelekeza madereva kuwa iwapo mtu anasubiri kuvuka kwenye kivuko wasimame kumpisha au pia kama watamkuta katikati au anamalizia kuvuka waache amalize kuvuka.
Lakini kwa madereva ‘vichwangumu’ hawazingatii. Huvuka kwa kasi, tena kwa kupiga honi
nyingi. Bodaboda, malori, mabasi ya abiria (ya masafa na daladala) na baadhi ya magari binafsi yakiwamo
ya serikali, ni vinara.
Mara nyingi utashuhudia madereva ‘wastaarabu’ na watii wa sheria wakipunguza mwendo
au kusimama kwenye vivuko, lakini madereva wababe na vilaza wa sheria hupita kwa kasi licha ya
kuashiriwa kusimama hali ambayo imekuwa ikihatarisha maisha ya watu.
Soma pia: Taa za Barabara ya Bibi Titi zawaibua watumiaji
Nawaita madereva vilaza, wasiozingatia udereva wa kujihami na kushindwa kutambua kuwa barabara zinatumiwa na watu wote wakiwamo watoto, wenye ulemavu, wazee, wagonjwa hata na walevi ambao wote wana haki ya kuishi.
Jicho langu linatamani kuona ikijengwa miundombinu mingi itakayowezesha waenda kwa miguu
kutembea barabarani bila hofu ya kugongwa na vyombo vya moto.
Vivuko vya juu ni sehemu ya suluhisho kwani huwezesha watu kwenda upande mwingine wa barabara. Hii itapunguza sana vifo na majeruhi vinavyosababishwa na kugongwa wakivuka barabara.
Ingawa katika baadhi ya maeneo yenye madaraja ya kuvuka kwa miguu wapo watumiaji ambao huyapa kisogo, haiondoi ukweli kwamba ni hatua mojawapo ya kunusuru maisha ya watu mijini.
Mfano ni maeneo ya Buguruni, Manzese (wilayani Ilala) na Mbezi Luis (Ubungo) katika daraja la kwenda Kituo Kikuu cha mabasi cha Magufuli ambako baadhi ya waenda kwa miguu huweka maisha yao rehani kwa kuvuka maeneo
yasiyostahili.
Hapa ndipo elimu zaidi inahitajika kuhusu usalama barabarani, ikibidi hatua zichukuliwe ili kila
Mtanzania afahamu kuwa sheria haiwahusu madereva pekee bali hata waenda kwa miguu ambao
wakati mwingine wanaweza kuwa chanzo cha ajali.
Likiachwa suala zima la kutoheshimu vivuko vya waenda kwa miguu, eneo lingine la kufanyia
kazi ni baadhi ya madereva na waendesha vyombo vya moto kuvamia njia za pembezoni, maalumu
kwa waenda kwa miguu.
Wakati sheria inamtaka mtembea kwa miguu apite upande wa kulia mwa barabara, bado hana
haki nao kwani pikipiki, maguta, malori na magari mengine ‘yenye haraka zaidi’ hupita tena kwa kasi
ya ajabu.
Waenda kwa miguu huwa na wasiwasi kwani hata wakati wa kuvuka barabara kubwa, hawawezi
kujihakikishia upande yanakotoka magari kwani ni kawaida kushuhudia magari, pikipiki zikivunja sheria
na kupita upande tofauti.
Kwa ujumla, sheria ya usalama barabarani inayowataka watumiaji wote wa barabara kuheshimu na
kufuata ishara zilizowekwa, imekuwa ikikiukwa, matokeo yake ni ajali zitokanazo na uzembe.
Katika maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kitaifa iliyoadhimishwa mwaka huu
mkoani Dodoma, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuka
milisha haraka mapitio ya Sheria ya Usalama Barabarani ikiwamo adhabu za makosa mbalimbali ya
barabarani.
Naunga mkono maagizo aliyotoa nikiamini yakitekelezwa ipasavyo, pia waenda kwa miguu
hawatapata mtihani mkubwa katika miji hususani Dar es Salaam.
Maana Dk Mpango alisisitiza wanaovunja sheria za usalama
barabarani wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria bila kujali ni wa gari la mtu binafsi, serikali au
taasisi ya umma, polisi iendelee kuimarisha doria, ifuatilie mwenendo wa madereva.
Alihimiza matumizi ya Tehama katika kudhibiti ajali na makosa mengine ya usalama
barabarani.