Wafanyabiashara mbogamboga wampa 5 Samia

DODOMA: WAFANYABIASHARA wa Soko la Bonanza-Chamwino jijini Dodoma, wameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa kufanikisha ujenzi wa eneo la Soko la Bonanza maalum kwa ajili ya wauza mbogamboga na matunda.

 

Pongezi hizo zimetolewa leo wakati wa ziara ya Mavunde ya kukagua ujenzi wa soko hilo na kuzungumza na wafanyabiashara wa soko la Bonanza.

Advertisement

Akitoa maelezo ya awali Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Bonanza, Goha Mwagai amesema ujenzi wa soko la mboga mboga na matunda utasaidia  kuwafanya wafanyabiashara hao kufanya biashara katika mazingira rafiki.

Pia, ameushukuru Serikali  kupitia Jiji la Dodoma  limetoa Sh milioni 50 na  Mavunde akichangia nguzo za chuma zenye thamani ya sh milioni  13 na mabati 400 yenye thamani ya  Sh milioni 13.8

 

Akizungumza na wafanyabiashara hao, Mavunde amesema ni dhamira ya Serikali na viongozi wote kuona wafanyabiashara hao wanafanya shughuli zao za kiuchumi katika mazingira rafiki na hivyo watahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kwa manufaa ya wafanyabiashara hao.

Amesema anafahamu kuwa ujenzi haujakamilika hivyo na amewaongezea  matofali 1500 na saruji mifuko 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kuweka sakafu ili pawe nadhifu.

Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Chamwino Jumanne Ngede ameahidi kusimamia mradi huo kwa karibu na fedha kutumika kwa malengo yaliyowekwa na si vinginevyo.

13 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *