Wafanyabiashara wahimizwa kutumia maonesho kutafuta fursa

MANYARA: WAFANYABIASHARA mkoani Manyara wamehimizwa kutumia Maonesho ya Nne ya Biashara, Viwanda, Madini, Kilimo na Utalii yanayoendelea katika Viwanja vya Tanzanite Kwaraa wilayani Babati, kutafuta fursa za uwekezaji, masoko, washirika wa biashara na wateja wapya.

Maonesho hayo yenye kaulimbiu “Uwekezaji Jumuishi, Ubunifu na Ustawi” yanalenga kuwa jukwaa la kujenga mahusiano ya kibiashara, kubadilishana maarifa na kuanzisha ushirikiano mpya wa uwekezaji.

Akifungua maonesho hayo leo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martine Shigela, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Shambani Mpendu, amesema maonesho hayo yanawapa wafanyabiashara fursa ya kutangaza bidhaa na huduma zao, kukutana na wanunuzi, kujifunza teknolojia mpya na kutafuta fursa za kupanua shughuli zao.

Mpendu amewahimiza washiriki kutumia maonesho hayo kwa malengo ya kibiashara yatakayozalisha matokeo chanya na kuchangia ukuaji wa shughuli zao.

Kwa upande wake, Meneja Uendeshaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Kanda ya Arusha, Cletus Mwakalinga, amewahimiza wananchi kutunza fedha kwa uangalifu na kuepuka kuziharibu kwa njia mbalimbali.

Mwakalinga amesema wananchi wanapaswa kuwasilisha katika benki za biashara fedha zilizochakaa au kuharibika ili ziweze kubadilishwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Amesisitiza kuwa ni kosa kuharibu fedha kwa makusudi, ikiwemo kuzichana au kuzichoma moto, akieleza kuwa kuna vigezo vinavyozingatiwa katika kupokea fedha zilizoharibika kwa ajili ya kubadilishwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button