Wageni wakutwa na biashara ‘haramu’ Kariakoo Dar

KAMATI Maalumu ya Ukaguzi wa Biashara zinazomilikiwa na wageni iliyoundwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Seleman Jafo imebaini biashara nyingi zinafanywa kinyume cha sheria na kanuni eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa kamati hiyo iliyoundwa Mei 5, mwaka huu, Thabit Massa alisema jana kuwa kamati ilikagua jumla ya biashara 108 na kubaini baadhi yake hazikuwa na leseni halali, na nyingine leseni zikiwa zimekwisha muda wake.

“Kati ya kampuni 53 zilizokaguliwa na FCC (Tume ya Ushindani), maduka tisa yalikutwa na bidhaa bandia na jumla ya bidhaa 6,621 zilikamatwa zikiwemo vesti, nguo za ndani, mitandio pamoja na viatu aina mbalimbali vilivyofikia 29,269,” alieleza Massa.

Alisema Jeshi la Polisi lilibaini wafanyabiashara 183 wanaofanya biashara kinyume na sheria wakitokea mataifa tisa ikiwamo China yenye raia 135, Watanzania 32, Kenya watano, Nigeria wawili, Misri wawili, Yemen wawili, India wawili, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mmoja.

Katika upande wa uhamiaji, alisema wageni wawili walifutiwa vibali na 12 waliondoshwa nchini, huku Idara ya Kazi ikifuta vibali vya wageni watano.

Kamati ilibaini pia kampuni 13 kati ya 83 zilizokaguliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kukiuka sheria za viwango au kukosa vibali.

Massa alisema kamati imependekeza marekebisho ya sheria ili kurahisisha usajili na kutoa fursa kwa wazawa kunufaika na rasilimali zao kama ilivyo katika mataifa mengine.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo alisisitiza kuwa serikali itachukua hatua stahiki za kisheria na kuwasilisha marekebisho bungeni.

Baadhi ya mapendekezo ya kamati ni kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili wa Kampuni, Sheria yaLeseni, Sheria ya Uhamiaji na Sheria ya Uwekezaji ambazo kwa sasa zimekuwa zikitumiwa kama mianya ya
kuingiza wageni kwenye maeneo yaliyopaswa kufanywa na wazawa.

Dk Jafo aliitaka kamati hiyo iendelee kukagua kila taasisi kwa eneo lake ili kuondoa wale wote wanaofanya biashara kinyume cha sheria na kanuni za nchi.

Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe kutoka FCC, TBS, Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Ofisi ya Rais Ikulu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Idara ya Uhamiaji, Idara ya Kazi, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara
Tanzania (TanTrade), Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button