Wagonjwa 500 watibiwa nyonga, magoti Mloganzila

DAR ES SALAAM; Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imehudumia wagonjwa takribani 500 kupitia huduma za kibingwa za upasuaji wa nyonga na magoti, ikiwamo upasuaji wa kubadilisha viungo vilivyoharibika na kuweka viungo bandia.

Huduma hiyo ilianza kutolewa hospitalini hapo mwaka 2020/2021 ikiwa sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya nchini na kupunguza changamoto zinazowakabili wagonjwa wenye matatizo ya nyonga na magoti.

Akizungumzia mafanikio hayo kuelekea kumbukizi ya miaka 27 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa aliyebobea katika nyonga na magoti, Dk Shilekirwa Makira amesema hospitali imepiga hatua kubwa eneo hilo.

Amesema mafanikio hayo yanaakisi kwa vitendo falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kupambana na maadui watatu wa maendeleo ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.

Alisema katika sekta ya afya, jitihada hizo zinaendelea kuonekana kupitia huduma zinazolenga kupunguza maradhi na kuboresha maisha ya wananchi.

“Wakati huduma hiyo inaanzishwa, hospitali ilikuwa bado haina wataalamu wa kutosha katika eneo hilo, lakini kwa sasa tumefanikiwa kuwa na wataalamu watano wanaoshughulikia upasuaji wa nyonga na magoti,” amesema.

Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada za hospitali na serikali katika kuwezesha wataalamu kupata mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuongeza ujuzi na uwezo wa kutoa huduma hizo.

Ameongeza kuwa hospitali imekuwa ikishirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi kupitia kambi za matibabu na mafunzo, hatua iliyosaidia kuongeza uzoefu wa wataalamu wa ndani na kuwahudumia wagonjwa wenye mahitaji hayo.

“Miongoni mwa wataalamu walioshirikiana na hospitali wanatoka Uingereza, ambako tayari zimefanyika kambi tatu za mafunzo na matibabu kwa Watanzania,” amesema.

Aidha, amesema wataalamu wa hospitali hiyo wamepata mafunzo katika nchi mbalimbali, zikiwamo Misri na China, kwa lengo la kuimarisha uwezo wao katika kutoa huduma za kibingwa za nyonga na magoti.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button