COMORO: SHIRIKA la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, limesema kuwa watu 25 wamepoteza maisha kufuatia kwa ajali ya boti iliyokuwa ikisafirisha wahamiaji haramu kati ya kisiwa cha Comoro cha Anjouan na kile cha Ufaransa cha Mayotte.
Katika taarifa hiyo, IOM imesema boti hiyo ilizama wiki iliyopita ikitokea Comoro kwenda Ufaransa wakati wakisafirisha wahamiaji haramu wanaopoteza maisha kila siku.
Katika tukio hilo, wavuvi waliwaokoa watu watano na wengine walishindwa kuokolewa.
“ boti hiyo ilibeba watu 30 wa mataifa tofauti wakiwemo wanawake na watoto,” walisema walionusurika .
Kwa mujibu wa ripoti maalum iliyotolewa hivi karibuni na baraza la seneti la Ufaransa imeeleza kuwa kati ya watu 7,000 hadi 10,000 wanapoteza maisha wakijaribu kuvuka kutoka Comoro kwenda Mayotte kati ya mwaka 1995 na 2012, lakini huenda idadi hiyo ikaongezeka.