Wahandisi wanawake kazi kwenu

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema serikali imeweka mazingira wezeshi kutoa fursa kwa wahandisi wanawake kushiriki utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi, matengenezo ya barabara na madaraja nchini.

Bashungwa ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh bilioni 840 kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya ambapo kazi hizo zitatekelezwa na makandarasi na wahandisi wazawa wakiwemo wanawake.

Bashungwa amezungumza hayo leo Agosti 21, mkoani Dar es Salaam wakati alipofungua kongamano la tisa la wahandisi wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), kupitia kitengo cha wanawake na kuwasisitiza wahandisi wanawake kuchangamkia fursa hizo.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa wazawa na hivyo kupitia mkakati wa Wizara ya Ujenzi wa wakushirikisha wakandarasi na wahandisi wazawa katika utekelezaji wa miradi ya barabara unatoa vipaumbele na fursa katika kuwahusisha wahandisi wanawake kikamilifu katika kutekeleza dhana ya ushirikishwaji katika miradi endelevu ya kimkakati na uwekezaji nchini”, amesema Bashungwa.

Ameeleza kuwa kila mwaka serikali imekuwa ikitenga takribani Sh bilioni 600 kwa ajili ya kazi za matengenezo ya barabara ambapo zinatoa fursa kwa makundi maalum ikiwemo kundi la wanawake kutekeleza kazi hizo kwa asilimia 100.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by HABARILEO (@habarileo_tz)

Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara ya Ujenzi imetenga miradi ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 120 za lami ambazo zitashindanishwa kwa makandarasi wa ndani pekee na zitatoa kipaumbele kwa wakandarasi wanawake pamoja na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 20, ambao umegawanyika katika sehemu nne za kilometa tano.

Habari Zifananazo

Back to top button