Waharibifu mazingira waonywa Mvomero

MOROGORO: MKUU wa Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Maulid Dotto amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji na misitu ya asili.
Aidha, amewataka wajenge tabia ya kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabiachi na kuondokana na changamoto za kimazingira ikiwemo ya ukosefu wa maji ya uhakika.
Dotto amesema hayo alipotoa salamu za Serikali ya wilaya katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mvomero kilichofanyika wilayani humo.
Amesema licha ya jitihada zinazoendelea kuchukuliwa za kulinda na kuhifadhi mazingira, misitu na vyanzo vya maji , bado kumekuwa na shughuli za kibinadamu zinazoharatisha na kujaribu mazingira, misitu na vyanzo vya maji.
Dotto amesema miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na kilimo, uanzishwaji wa makazi, ufugaji holela, uchomaji wa moto, uvunaji wa mkaa na mazao ya misitu na uchimbaji holela wa madini.
Mkuu wa wilaya amesema shughuli hizo zinazofanyika kinyume na sheria katika baadhi ya maeneo zimekuwa zikididimiza jitihada za upatikanaji wa maji hasa katika taarafa ya Mvomero na Turiani.
“Rai yangu kwenu Madiwani ni kuendelea kuhamasisha wananchi katika maeneo yenu ni kulinda na kuhifadhi mazingira, misitu na vyanzo vya maji,”amesema Dotto.
Mkuu wa wilaya pia amehimiza Madiwani hayo kuhamasisha zoezi la kupanda miti, kuhifadhi uoto wa asili na kudhibiti shughuli zote za kibinadamu zinazoatjiri mazingira na vyanzo vya maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Koira Majuka, amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa hatua anazozichukua kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira linapewa kipaumbele wilayani humo .
Majuka amesema hatua hizo ni kuweza kukabiliana na athari za mafuriko yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji ikiwemo kilimo na uchimbaji holela wa madini
Amesema kuwa athari za uharibifu wa mazingira zimeonekeana moja kwa moja baada ya kutokea kwa mafuriko katika maeneo tofauti na hatua zilizochukuliwa na kamati ya maafa ya wilaya zimeonesha nia ya dhati ya kudhibiti hali hiyo isitokee nyakati nyingine.
Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Mziha, Denis Ignas amesema changamoto ya uhalibifu wa mazingira imeanza kupunguza taratibu baada ya wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hasa katika matumizi ya teknolojia na nishati safi ya kupikia.
Ignas amesema kutokana na mwitikio wa wananchi kuanza kutumia nishati safi ya kupikia aliiomba Serikali kuongeza juhudi za kuwafikishia nishati hiyo wananchi wa vijijini kwa gharama nafuu.
“Serikali iweke mkakati wa kukabiliana na changamoto hii anayoieleza mkuu wa wilaya na kila diwani anapokuwa kwenye mkutano ya wananchi atumie fursa hiyo kuwaelimisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira,”amesema Ignas.
“….tuwaelimishe wananchi wetu waache kutumia nishati chafu, ila ombi langu ni kwa Serikali na wadau ni kusaidia kufikisha nishati safi ya kupikia vijijini kwa gharama nafuu kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini,”amesema Diwani Ignas.



