Wahimizwa kupanda na kutunza miti

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dk Khatibu Kazungu amewataka wadau wa mazingira kushiriki katika upandaji na utunzaji wa miti katika mazingira waliyopo ili kutekeleza Mkakati wa Utekelezwaji wa Sera ya Taifa ya Uhifadhi wa Mazingira wa mwaka 2020/21.

Dk Kazungu ameyasema hayo jijini hapa wakati wa upandaji miti ikiwa ni mojawapo ya shughuli za Maadhimisho ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Alisema moja ya changamoto za uhifadhi wa mazingira nchini ni ukataji miti na uharibifu wa misitu.

“Taarifa ya tatu ya mazingira nchini ya mwaka 2019 inaonesha kuwa takribani hekta 469,420 za misitu kwa mwaka hupotea kutokana na utegemezi mkubwa wa nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia, kilimo na ufugaji wa kuhamahama.”

“Pia inakadiriwa kuwa ili kurejesha eneo la misitu linalopotea kila mwaka, inahitajika kupanda na kutunza miti katika eneo lenye ukubwa wa hekta 185,000 sawa na miti 2,280,000 kwa mwaka kwa muda wa miaka 17 mfululizo,” alisema.

Aidha, Dk Kazungu alisema serikali imeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uhifadhi wa Mazingira kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2032.

Awali, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mathew Maimu alisema utekelezaji wa haki za binadamu ni muhimu kwa mazingira salama ili kuwezesha jamii kuishi mahali pa utulivu na usalama na kuwezesha kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa maendeleo ya nchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa upandaji miti na kuwasihi kuwa katika maadhimisho hayo ya kutimiza miaka 20 wajitahidi kutatua changamoto za wananchi wa Dodoma hasa kwenye sekta ya ardhi na mirathi.

Katika utaratibu wa upandaji miti, miti 600 ya matunda na kivuli imepandwa katika eneo la ekari mbili.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button