WANAFUNZI waliohitimu kidato cha nne wameshauriwa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ili wapate ujuzi zaidi kipindi wanachosubiri kuendelea na masomo katika maeneo mbalimbali.
Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), Sitta Peter ametoa ushauri huo alipozungumza na HabariLeo mkoani Dar es Salaam.
“Kuna vijana wengi wamemaliza kidato cha nne na wanatarajia kujiunga na masomo mengine kwenye ngazi nyingine,
“Mfano wapo ambao watakwenda kidato cha tano, wapo ambao watakwenda kwenye vyuo mbalimbali na kuna wengine wanaweza wasipate hizo fursa,
“Sasa tunawaambia wakati wakiwa katika kipindi hiki cha mpito kabla matokeo kutoka na kabla ya kupangiwa maeneo mengine au ngazi nyingine za mafunzo watumie fursa hii badala ya kukaa nyumbani au kuingia kwenye kusoma masomo ya tuition,” amesema.
Amesema wanafunzi hao watumie muda huu kusoma kozi za muda mfupi za ufundi stadi ambazo ikitokea amechaguliwa kujiunga kidato cha tano, anakwenda akiwa tayari na ujuzi wake.
“Tuna fursa nyingi na fani nyingi za ufundi ambazo anaweza akachagua anataka ipi na wakati wa likizo akirudi anaweza kufanya shughuli zinazofanana na fursa hizo,” amesema.
Comments are closed.