Wahitimu kidato cha sita waitwa jeshini
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limewaita vijana wote waliomaliza kidato cha sita mwaka 2023, kuripoti katika makambi ya Jeshi hilo kwa ajili ya mafunzo ya kwa mujibu wa sheria kuanzia Juni Mosi hadi 11 mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo Mei 25, 2023 na Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena wakati wa kutoa taarifa iliyotolewa kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi hilo, Meja Jenerali Rajabu Mabele.
Amesema kuwa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho wanatakiwa kuripoti katika kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa Jamii hiyo.
“Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele amewakaribisha vijana wote waliohitimu kidato Cha sita mwaka 2023 kuungana na vijana wenzako Ili kujengewa uzalenzo , umoja wa kitaifa, kufundishwa stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa lao.”Amesema Mabena
Aidha, Brigedia Jenerali Mabena pia amewataka vijana hao kuja na bukta ya rangi ya blue iliyokolea yenye kiuno iliyo na mfuko mmoja nyuma, urefu unaoishia magotini isiyo na zipu.
Vingine ni tisheti ya rangi ya kijani, raba za michezo zenye rangi ya kijana au blue, shuka mbili za kulala zenye rangi ya bluu bahari, suruali ndefu za rangi nyeusi na nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa mikoa yenye baridi.
Pia wametakiwa kwenda na trakisuti ya rangi ya kijana au bluu, nyaraka zote zinazohitajika katika usajili wa kujiunga na elimu ya juu, zikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya kuhitimu kidato cha nne.
Brigedia Jenerali Mabena amesema vijana hao wanahitajiika kwenda na nauli za kwenda na kurudi nyumbani.
Amesema orodha ya majina na makambi waliyopangiwa na maeneo yaliyopo yanapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.
jkt.go.tz.
Amesema utaratibu kupata walizopangiwa umerahisishwa ambapo kijana ataandika majina yake matatu aliyotumia kwenye mtihani na kupata jina la kambi alilopangiwa na eneo lilopo.