WAHITIMU wa Chuo cha Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Mtwara wameombwa kutumia elimu waliyoipata kwa ajili ya kupambana na umaskini kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo Novemba 15, 2024 katika Mahafali ya 22 ya Taasisi hiyo iliyopo Mjimwema Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya amesema hatua hiyo ya kuhitimu iwe chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma ili waweze kushindana katika soko la ajira na kujiajiri ili kupambana na umasikini.
Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 408 wamehitimu wakiwemo wanaume 205 na wanawake 203.
Mwaipaya amewataka wadau wa maendeleo kuchangamkia fursa ya uwepo wa chuo hicho kwa ajili ya kujenga hosteli ili kukuza pato.
“Uwepo wa chuo kwenye mkoa wa Mtwara ni fursa ya kuchechemua uchumi na kuchangamsha mji pia niwatake wazazi na walezi kutumia fursa ya uwepo wa chuo hiki kwenye mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kupata elimu”amesema Mwaipaya.
Ameongeza kuwa “Tukiangalia kwa asilimia kubwa ya wahitimu wote wanafunzi kutoka mtwara ni wachache sana, tulitaraji tuweza kuona wanafunzi wengi wanatoka hapa kutokana na huduma hii kusogezwa karibu nasi lakini wanafunzi wengi wametoka nje ya Mtwara, tutumie fursa hii ambayo serikali yetu imeiyona na kutusogezea”
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara TIA Nicolous Shombe amesema serikali kupitia Wizara ya Fedha imetenga jumla ya shilingi bilioni 58.1 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika kampasi za TIA hatua iliyopelekea ongezeko la udahili.
Yusuph Yusuph ni miongoni mwa wanafunzi waliyohitimu chuoni hapo ambaye amewataka wahitimu wenzake kutokata tamaa kutokana na changamoto ya ajira iliyopo kwani dunia ya sasa inaamuliwa kwa ubora alio nao mtu na kukufikisha unapopataka