Waipongeza serikali mageuzi sera ya kodi, sekta ya fedha

WACHAMBUZI wa uchumi na fedha wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa mageuzi ya sera ya kodi na sekta ya fedha hali iliyoitoa kimasomaso sekta binafsi.

Wamesema kuimarika kwa sekta binafsi kunatoa mwanya kwa sekta ya ajira kuimarika kwa kuwa sekta binafsi ndio kichocheo na uti wa mgongo wa upatikanaji wa ajira Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti (Repoa), Dk Donald Mmari ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya uchumi aliliambia HabariLEO kuwa mabadiliko ya sera ya kodi ambayo ni utashi binafsi wa Rais Samia Suluhu Hassan yamesababisha kufanyika kwa makadirio sahihi ya kodi bila kumwonea mtu hali ambayo imeamsha ari ya biashara na uwekezaji nchini.

Aliongeza kuwa kabla ya Rais Samia kuingia madarakani, sekta binafsi ilipitia wakati mgumu na kusababisha wafanyabiashara kukata tamaa lakini baada ya kuingia Serikali ya Awamu ya Sita, sekta binafsi ilichukua mikopo kwa wingi kuimarisha biashara.

“Awali kulikuwa na malalamiko kuhusu sera ya kodi ambapo walilipa kodi ambayo sio ile waliostahili kulipa na kusababisha wafanyabiashara wengi kufunga biashara zao,” aliongeza.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Profesa Humphey Moshi alisema sekta binafsi imeimarika katika mikopo kutokana na mageuzi ya sekta ya fedha yaliyofanywa na serikali ambapo madeni chechefu yalipungua na kutoa mwanya kwa wakopaji kuchukua mikopo.

Kwa upande wake, Mchambuzi wa Siasa na Uchumi, Gabriel Mwang’onda pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika sekta hizo, aliishauri serikali kuangalia namna ya kupunguza zaidi riba ili haki ya kuchukua mikopo iwe ya watu wa hali zote.

“Kwa kufanya hivyo, sekta binafsi itaendelea kuongeza ajira nchini kwa sababu miradi mingi itaendelea kuongezeka kutoka katika taasisi, kampuni na watu binafsi,” aliongeza.

Habari Zifananazo

Back to top button