Wajadili uchorongaji visima Mnazi Bay
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imekutana na uongozi wa Kampuni ya Maurel et Prom Exploration Production Tanzania Ltd inayosimamia kitalu cha Mnazi Bay kwa lengo la kujadili utekelezaji wa uchorongaji wa visima vitatu vya gesi asilia unaotarajiwa kuanza mwakani.
Wajumbe kutoka pande hizo akiwemo meneja wa utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia kutoka PURA, Simon Nkenyeli na meneja mkuu wa M&P, Sylvain Pichelin walikuta katika ofisi za mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam mapema wiki hii kujidili namna mradi huo utakavyoweza kutekelezeka kwa ufanisi.
Katika kikao hicho, Pichelin alifafanua bajeti ya mradi unaotarajiwa kugharimu Dola milioni 80.2 kabla ya PURA kutoa idhini ya mpango huo.
Kati ya visima vitakavyochimbwa, visima viwili (MB5 na MS2) vitakuwa visima vya uzalishaji (infill) wakati kisima kimoja (Kasa) kitakuwa kisima cha utafutaji.
Kuelekea utekelezaji wa mradi, tathmini ya athari kwa mazingira imekamilika na zoezi la fidia kwa wananchi watakaopisha mradi linatarajiwa kuanza mapema mara baada ya uhakiki kukamilika.
PURA na M&P zilitumia fursa hiyo kujadili ushiriki wa Watanzania na watoa huduma wa
Mwakilishi wa PURA aliitaka M&P kuhakikisha inazingatia matakwa ya Sheria kuhusu ushiriki wa Watanzania huku akiweka bayana kuwa mamlaka hiyo inafuatilia kwa karibu kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wazawa na watoa huduma wanashiriki kikamilifu.
SOMA: Dk Biteko atoa maagizo fedha gesi asilia
Kitalu cha Mnazi Bay kina visima vitano vinavyozalisha gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo milioni 74.24 kwa siku (kwa mwezi Septemba)
Wabia katika Kitalu hicho kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ni M&P (ambaye ni mwendeshaji) mwenye ushiriki wa asilimia 60 katika shughuli za uzalishaji na TPDC mwenye asilimia 40.
Uchorongaji wa visima vitatu vipya utawezesha kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa taarifa za kijiolojia kuhusu rasilimali iliyopo katika Kitalu hicho.