Wajane 100 wapatiwa kadi za NHIF Mtwara

WAJANE 100 wamepatiwa kadi za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutoka Taasisi isiyokuwa ya serikali mkoani Mtwara ya Joel Nanauka Foundation zilizogharimu Sh milioni 30.

Akizungumza leo katika ghafla hiyo fupi ya ugawaji wa kadi hizo, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Joel Nanauka amesema wameguswa kufanya hivyo kutoka na changamoto nyingi wanazokutana nazo wanawake hao kwani wengi wao hukosa msaada kwenye familia zao.

Amesema wamewakatia bima hizo kwa ajili ya kuwasaidia kupata matibabu ndani na nje ya Mkoa wa Mtwara kwa sababu ni bima kubwa hivyo wanaweza kwenda hadi hospitali za rufaa, ghafla iliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani humo.

Advertisement

“Mtwara tuna wajane 100 lakini pi tuna mikoa mingine na kwa takwimu zinaonyesha tanzania mzima tuna wajane karibu laki nane na elfu themanini ambao karibia asilimia 3.1 ya wananchi wote wa Tanzania”

Aidha kwa mkoa mzima wa mtwara pekee kuna wajane 5,000 na kikubwa kinachofanywa taasisi hiyo ni kuona wanawafikia wadau wengine kuja kuwasaidia wajane hao.

Hata hivyo wajane hao wengi wao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo magonjwa sugu kama vile kansa, kisukari na mengine yanayohitaji msaada mkubwa ikizingatiwa wengi wao hawana kipatao cha kijitosheleza.

“Nia yetu ni kuona tunapata wadau wengine wa kuweza kutusaidia, sisi kama Nanauka Foundation tumetoa sehemu hii lakini tunatamani wadau wengine watuunge mkono ili tuweze kutoa kwa wengi zaidi “amesema Joel.

Meneja wa NHIF mkoani humo, Adolf Kahamba amewasisitiza wajane hao kutotumia kadi hiyo kwa mtu zaidi ya mmoja na zipo tayari kufanya kazi kuanzia hivi sasa na ni za kipindi cha mwaka mmoja.

‘”Nawasihi hiyo kadi ni ya kwako usimwazimishe mtu mwingine nawasihi sana mama zangu itakuwa umetenda kosa kwasababu huyo utakaemwazimisha kadi akikamatwa hiyo kadi itafungiwa”amesisitiza

Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Sixmund John amesema ni faraja kubwa kwa wanamtwara kuona wadau kama hao wanafanya mambo mengi ya kijamii ikiwemo hilo lililofanyika la kuona na kutambua mahitaji ya watu wenye mahitaji wakiwamo wajane hao.

Mratibu wa Wajane Kanda ya Kusini, Sesilia Erio amewaomba wajane hao kuendelea kutambua mchango mkubwa unaofanywa na taasisi hiyo kwa mtu au watu pamoja na vikundi mbalimbali ikiwemo wajasiliamali na kutoa shukrani kutokana na vile taasisi hiyo inavyojali makundi hayo.

Baadhi ya wajane hao akiwemo Felister Joseph mkazi wa kata ya majengo kwenye manispaa hiyo, “Tunafurahi sana wajane kwa msaada huu mkubwa wa kutusaidia matibabu kwasababu wakati mwingine tunaumwa lakiki hatuna ela matibabu”