Wajasiriamali wapewa mafunzo ubora wa masoko

ARUSHA: ZAIDI ya wajasiriamali 300 wa matunda na mbogamboga kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wamepatiwa mafunzo salama, ubora, masoko na ufungashaji wa mbogamboga yaliyoandaliwa na Shirika la Viwanda Vidogo Mkoa (SIDO) Mkoa wa Arusha.
Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Kimataifa la World Vegetable Centre pamoja na Shirika la Kilimo Trust wakati wa kilele cha kufunga mafunzo hayo.
Ofisa kutoka Trust ,Salumu Isaka alisema yametokana na utafiti wa awali ulifanywa ambao ulibaini usalama mdogo wa chakula kwa wafanyabiashara hao hivyo kuwawezesha mafunzo ili kufanya shughuli zao kwa ubora unaotakikana.
“Leo hii tumekuwa na shughuli ambayo imehusisha wauzaji wa mboga mboga kutoka soko kuu,kilombero na samunge ambapo mafunzo yamefanyika kwa siku tano,yalilenga kuboresha biashara zao,”
Pia amesema mafunzo hayo yanawawezesha kuzingatia usafi wakati wanafanya shughuli ya uuzaji wa mboga mboga,kuweka lebo katika bidhaa zao kufikia masoko zaidi ya haya ambayo wanayo ili kuongeza kipato zaidi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamefikia wauza mbogamboga 300 katika mikoa ya Kilimanjaro 150 na 150 Mkoa wa Arusha, ni muendelezo wa utekelezaji wa miradi ambapo kwa ujumla wamefikiwa wakulima 6000, pamoja na wauzaji mboga mboga ambapo utafiti wa awali ulionyesha namna ambavyo wanafanya shughuli za uuzaji wa mboga mboga zinapangwa chini na mazingira sio rafiki kwa kuzingatia afya ya mlaji.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, John Mkude amesema usalama wa chakula ni lazima kuzingatiwa kwa kuwa serikali inaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara katika wilaya ya arusha mjini na kuhakikisha wananchi wanatumia fursa mbali mbali kujiingizia kipato.