Wajenga maktaba 300 kusaidia kuinua taaluma
GEITA; SHIRIKA lisilo la kiserikali linalosaidia maendeleo ya taaluma nchini, Room To Read (RTR), limejenga maktaba 300 kwenye maeneo mbalimbali ili kuongeza hamasa ya watoto kujifunza.
Ofisa Mradi wa shirika hilo, Mariam Kumbaye amesema hayo katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Global Action Week for Education (GAWE) yanayoendelea mjini Geita.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya kampeni ya soma na maktaba inayolenga kuwaimarisha watoto katika stadi za ujifunzaji ambazo ni Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), ili waweze kubobea kwenye nyanja tofauti.
“Tupo kuhamasisha wadau wengine wote kuendelea kusapoti usomaji wa wanafunzi wetu, lakini pia kuendelea kusapoti maktaba katika nyanja zote mbili, maktaba ya kawaida na maktaba mtandao,” amesema.
Amesema mradi umesaidia kupunguza tatizo la utoro shuleni na kuepuka matumizi mabaya ya muda, kwani muda mwingi watoto wanavutiwa kuutumia zaidi katika vyumba vya maktaba hizo.
Ofisa Mradi wa Elimu kwa Msichana kutoka shirika hilo, Chonge Zuberi amesema kampeni ya ujenzi wa maktaba inaenda sambamba na uwezeshaji wa mabinti wasikatishe masomo kwa sababu yoyote.
“Kwanza ni utoaji wa stadi za maisha kwa wasichana, cha pili ni utoaji wa ushauri nasaha kwa wasichana na cha tatu ni ushirikishaji wa familia na jamii za hawa wasichana wanapotokea,” amesema.
Amesema mpaka sasa mradi umefikia mabinti takribani 13,000 wa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro na kusaidia kupunguza mdondoko wa wanafunzi kwa asilimia nne.
“Tunaamini binti akipewa stadi sahihi ataweza kufikia malengo yake, ataweza kuhitimu elimu ya sekondari, lakini pia ataweza kufanya mabadiliko chanya,” amesema
Naibu Katibu Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Charles Msonde amesema serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia na kushirikisha wadau ili kuinua sekta ya elimu nchini.
Dk Msonde amesema mpaka sasa serikali imeboresha shule zote za sekondari za kata zilizokuwepo na kujenga shule mpya na inafuatilia na kutatua changamoto za kujifunzia na ufundishaji kwenye shule za umma.